Tuesday, 22 March 2016

WANAJUMUIYA WA KIKUNDI CHA UMOJA GROUP MKOANI GEITA KUPEWA PIKIPIKI NA DIWANI WA KATA YA BUKOLI.


Diwani wa kata ya Bukoli wilayani Geita Mhe.Faraj Rajab Seif  amewaahaidi usafiri   wa  pikipiki wanajumuiya ya kikundi cha kijamii kiitwacho “UMOJA GROUP” kilichopo kijiji cha Bugogo, kata  ya Bukoli ndani ya siku 30 toka machi 19, 2016.


Ahadi hiyo ilitokana na ombi lililotolewa na kikundi hicho siku hiyo kikundi kilipokuwa na sherehe ya mwaka kama ilivyo ada ya kikundi hicho.

Akiongea kwa furaha kwa niaba ya kikundi hicho, msemaji wa kikundi Gerard Mellato ambaye pia ni mwenyekiti, alimshukuru Mh. huyo kwani hayuko nyuma katika kuhakikisha wananchi wake wanasonga mbele kimaendeleo kwani kikundi hicho hujishughulisha na kuhudumia watoto waliyo kwenye mazingira hatarishi kwa kuwapa mahitaji ya shule.

Aidha Lawrence  Kalabezile kwa niaba ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya pia hakuwa nyuma kuonesha namna alivyoguswa kwa kuchangia lita 15 za petroli  ya kuanzia pindi  watakapokabidhiwa chombo hicho cha usafiri na pia aliwahaidi wanakikundi hao kuwa ofisi yake itakuwa tayari kushirikiana nao na tayari  ilishamtuma mtaalam wa maendeleo ya jamii katani  hapo kwa ajili ya kuhakikisha vikundi kama hicho vinasonga mbele.

Jumla ya fedha laki moja na sitini (160,000/=) zilichangwa kama fedha ya  mafuta (petroli) na wadau mbali mbali wakiwemo wananchi, waalimu, watendaji wa vijiji, na kata, mahakimu na wafanyabiashara.

Kikundi hicho kwa sasa kinahudumia watoto 12  kwa kuwalipia ada na mahitaji ya shule na kina malengo ya kuhudumia watoto 50 ifikapo 2017.
Kimetoa rai kwa wadau mbalimbali kujiunga na kutoa michango yao ya hali na mali kwa kikundi hicho kwani kimeonesha mfano bora katika kata ya bukoli pia kina mpango wa kuanzisha shule ya awali ili kuokoa jamii ya wanabukoli hasa watoto waishio kwenye mazingira magumu


No comments:

Post a Comment