Mwalimu mmoja wa Shule Sekondari Nyugwa Mkoa
wa Geita anadaiwa kutoroka katika kituo chake cha kazi kwa tuhuma za kumpa
mimba mwanafunzi wake wa kidato cha tatu.
Inadaiwa baada ya mwanafunzi huyo (jina
linahifadhiwa) kubainika kuwa na ujauzito, mwalimu huyo aliamua kushirikiana na
baadhi ya watumishi wa Kituo cha Afya cha Kharumwa kutoa. Inadaiwa Machi 3,
ndiyo mimba hiyo ilitolewa kwa ushirikiano wa daktari na muuguzi waliokuwa
zamu.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa shule hiyo,
Henrick Jembe alidai Februari 18, mwanafunzi huyo aliomba ruhusa kwenda
hospitali akidai anaumwa.
“Ingawa sikuwapo shuleni siku hiyo, lakini
kumbukumbu zinaonyesha mwanafunzi huyu alipewa ruhusu baada ya kukamilisha
utaratibu ikiwamo kuandikiwa daftari la kumuwezesha kupatiwa matibabu,” alidai mkuu huyo na kuongeza:
“Alisindikizwa na wanafunzi wenzake wawili, mmoja
wa kiume na mwingine wa kike.”
Alidai waliporejea shuleni, mwanafunzi huyo
alisema baada ya vipimo alikutwa na vimelea vya malaria, hivyo akaruhusiwa
aende nyumbani kupumzika.
“Lakini baada ya siku mbili nilipokea wito kutoka
polisi nikitakiwa kufika na mwalimu anayetuhumiwa ambaye siku hiyo alikuwa na
kazi ya kushughulikia chakula cha wanafunzi, ikabidi niende mwenyewe na kukuta
maelezo kuwa mwanafunzi wangu ana ujauzito na anayetuhumiwa ni huyo mwalimu,” alisema Jembe na kuongeza:
“Nadhani alipopata taarifa kuwa anatuhuma hizo
aliamua kukimbia na mpaka sasa hajulikani alipo.”
Katibu Mkuu Idara ya Utumishi wa Walimu wilayani
hapa, Aron Andrew alisema baada ya kumhoji mwanafunzi huyo alibaini kuwa
alianza uhusiano wa mapenzi na mwalimu wake tangu mwaka jana.
“Alisema baada ya kutolewa mimba, mwalimu wake
alimsafirisha hadi jijini Mwanza kwa mtu aliyemtambulisha kwake kuwa ni dada wa
mtuhumiwa ili ajiuguze huku akiendelea kunywa dawa alizoandikiwa hospitali,”alisema
Hata hivyo, alisema hawawezi kuchukua hatua
yoyote dhidi ya mwalimu huyo kwa sasa kwa sababu wanasubiri taarifa kutoka kwa
mwajili wa mwalimu huyo ambaye ni mkurugenzi.
Alisema mwajiri huyo akitoa taarifa hatua za
kinidhamu zitachukuliwa dhidi mwalimu huyo kwa kuwa amekiuka sheria na kanuni
za utumishi wa umma.
Kaimu Mkurugenziwa wa Halmashauri ya Wilaya ya
Nyang’hwale, Venance Ngeleuya alisema ofisi yake pia haijapokea taarifa za
tuhuma hizo na kusisitiza watafuatilia.
Kaimu Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk Lutale
Josephat alisema ofisi yake itachukuwa hatua kama itathibitika kuwa baadhi ya
watumishi wa kituo cha afya cha Kharumwa walishiriki kumtoa mimba mwanafunzi
huyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale,
Ibrahimu Marwa alisema amewaagiza polisi wilayani hapa kumsaka na kumtia
mbaroni mwalimu huyo ili afikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya tuhuma
zinazomkabili.
No comments:
Post a Comment