Thursday, 3 March 2016

TANZANIA YAPOKEA MBWA WA KUNUSA KUBAINI BIDHAA HARAMU.

Visa vya usafirishaji wa bidhaa zilizopigwa marufuku kama vile zile zilizotengenezwa kutokana na Pembe na Ngozi ya wanyama wa Pori pamoja na mihadarati vimekuwa vikikithiri kutokana na kutokuwepo kwa mbwa maalum wa kunusa na kukagua bidhaa zinaposafirishwa kupitia viwanja vya ndege au Bandari.

Tanzania ni mojawapo ya mataifa yalioathirika kutokana na usafirishaji wa bidhaa aina hizo kinyemela. Hata hivyo hali hii huenda ikakoma kwani Serikali ya Tanzania sasa imepokea mbwa maalum wa kuwasaidia maafisa wa usalama na wakaguzi katika operesheni za kunasa bidhaa zilizopigwa marufuku.
Serikali ya Marekani kupitia Ubalozi wake wa Dar es Salaam, imetoa msaada wa Mbwa wanne na Mafunzo yaliyofanyika katika Chuo cha Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani (CBP).
Mbwa hao watasaidia Usalama katika Viwanja vya Ndege na Bandari kwa kubaini bidhaa haramu zinazovushwa katika maeneo kama hayo zikiwamo nyara za serikali na madawa ya kulevya.
Askari wanne watanzania wanaowasimamia mbwa hao wanatoka katika katika Kikosi cha Mbwa na Farasi na wamepata mafunzo na kufuzu katika chuo kilichoko El Paso, Texas Marekani.
“Ni msaada ambao umekuja wakati mzuri, ambapo wanyama pori maisha yao yako hatarini kuliko wakati wowote huko nyuma.” Alisema Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania, Profesa Jumanne Maghembe.
Bi Virginia Blaser Balozi Msaidizi wa Ubalozi wa Marekani alisema watu wanaojihusisha na Biashara haramu hawajali juu ya Tanzania na Watu wake bali wanajali Pesa tu ndiyo maana Marekani imeamua kusaidia kupambana na hali hiyo ili watu hao wakumbane na mkono wa Sheria.



No comments:

Post a Comment