Friday, 15 April 2016

RAISI WA SUDAN KUSINI SALVA KIIR AWASILI NCHINI TANZANIA KWA ZIARA YA SIKU MOJA



Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Bi Mindi Kasiga amesema Rais Kiir anafanya ziara ya kikazi ya siku moja ambapo anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sudan Kusini ilikubaliwa kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika mkutano wa wakuu wa nchi wa EAC uliofanyika jijini Arusha nchini Tanzania mwezi Machi 2016, tangazo lililotolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa imesema Sudan Kusini ina fursa nyingi za kiuchumi ambazo zinaweza kuzifaidisha nchi wanachama wa EAC ikiwemo Tanzania endapo mipango madhubuti itawekwa kuzichangamkia.


Taarifa hiyo imesema fursa hizo ni pamoja na biashara kwa kuwa karibu kila bidhaa inayotumika nchini Sudan Kusini inaagizwa kutoka nje ya nchi hiyo kwa kuwa inakabiliwa na uhaba wa chakula, huduma za kibenki, bima na wataalamu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment