Takukuru imeanza
kuchunguza taarifa kwamba Waziri wa Ardhi, William Lukuvi alikataa kupokea
rushwa ya Sh5 bilioni iliyotaka kutolewa na wafanyabiashara wawili wakubwa ili
kuwapitishia mradi wa Sh84 bilioni.
Katika mahojiano
na gazeti la Mwananchi hivi karibuni, Waziri Lukuvi alisema
kwamba lengo la wafanyabiashara hao ilikuwa ni kufanikisha mpango wao wa
kuiuzia Serikali ardhi kwa bei kubwa kwenye eneo linalotakiwa kujengwa mji wa
kisasa wa Kigamboni.
Licha ya kukataa
kutaja majina ya wafanyabiashara hao, Lukuvi alisema mtandao huo wa
wafanyabiashara ni hatari na unaweza kusababisha mtu ashindwe kufanya kazi ya
wananchi iwapo ataendekeza rushwa.
Jana, Mkurugenzi wa
taasisi hiyo, Valentino Mlowola alisema kutokana na taarifa ya kiongozi huyo,
ofisi yake iliamua kuchukua chanzo hicho na kuanza kazi ya uchunguzi.
Hata hivyo, Mlowola
hakutaka kuweka wazi kazi ya uchunguzi huo imeanza lini wala ilipofikia.
“Kueleza tumeanza lini hilo ni suala la
kiufundi, tumeshaanza kushughulikia,” alisema Mlowola ambaye Rais John
Magufuli amemuidhinisha rasmi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo baada ya
kukaimu kwa miezi kadhaa.
Katika ufafanuzi wake,
kamishna huyo wa zamani na mkurugenzi wa Intelijensia ya Makosa ya Jinai katika
Jeshi la Polisi, alisema taasisi hiyo kwa sasa imekuwa ikichukua tuhuma yoyote
ya rushwa kutoka chanzo chochote baada ya kuripotiwa.
Katika mahojiano hayo,
Waziri Lukuvi alisema wafanyabiashara hao waliwaeleza marafiki zake wa karibu
kuwa wangempa rushwa.
Mji huo mpya wa
Kigamboni unajumuisha kata za Kigamboni, Tungi, Vijibweni, Mjimwema, Kibada,
Somangila na eneo lote hilo lina ukubwa wa takribani ekari 6,000.
Awali mradi huo
ulitarajiwa kugharimu Sh13 trilioni ambazo zingetolewa na Serikali, lakini
ikaamua kushirikisha sekta binafsi ili kuujenga na Serikali ishughulikie
uwezeshaji wa awali.
Lukuvi ambaye
alihamishiwa Wizara ya Ardhi mapema mwaka jana na kubakizwa katika wizara hiyo
na Rais Magufuli, alisema amegundua kuna mtandao mkubwa wa rushwa unaoanzia
ngazi ya halmashauri mpaka wizarani ambao unahusisha maofisa wa Serikali na
viongozi wa wizara.
“Kama ukiwa na tamaa huwezi fanya kazi
uliyotumwa. Kuna wakati walikuja ni wafanyabiashara wawili wakubwa na kutaka
wanipe Sh5 bilioni ili nikubali kupitisha mradi wao wa mabilioni ya shilingi na
walitangaza kwa marafiki zangu kuwa wangenipa fedha, lakini hapa hawawezi,” alisema Lukuvi.
Aliongeza: “Wakati naingia tu wizara hii nilikuta
harakati za kukamilisha mradi wa Kigamboni ukiwa katika hatua za mwisho na kila
kitu kilikuwa kimekamilika. Lakini nilipopitia vizuri nilikataa kuwalipa
wafanyabiashara hao. Cha ajabu hazikupita siku mbili walipata taarifa wakaja
mbio kutaka kuniona.”
Kwa mujibu wa Waziri
Lukuvi, wafanyabiashara hao walitaka walipwe Sh141 milioni kwa kila ekari
wakati wao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa Sh5 milioni kwa ekari, jambo
ambalo alisema lilishapitishwa awali.
“Niligundua pale kuna udanganyifu na wizi
mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue kutoka kwa wananchi ekari moja kwa Sh5
milioni, kisha Serikali tumlipe Sh141 milioni kwa ekari kwa kuvuka pantoni tu.
Ni wizi mkubwa.
"Kama kweli Serikali ina fedha hizo kwa nini
tusimlipe mwananchi moja kwa moja?” alihoji.
Waziri Lukuvi alisema
endapo njama hizo zingefanikiwa, Serikali ingetumia zaidi ya Sh84 bilioni
kuwalipa wawekezaji hao hewa kwa kuwa mmoja anamiliki takribani ekari 200 na
mwingine 400.
“Niliwaambia Serikali haiwezi kuwalipa fedha hizo na badala yake waende
kuiendeleza ardhi wenyewe kulingana na mradi unavyotaka. Walitaka kutajirika
kwa ujanja ujanja,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Eti walidai wamekopa fedha benki kwa ajili ya
mradi huo. Haiingii akilini mtu utumie Sh5 milioni, halafu uje uvune mabilioni
ya fedha kwa kuvuka pantoni tu.”
No comments:
Post a Comment