Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka.
Hatima ya kesi ya
Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka kupinga kuilipa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) zaidi ya Sh500 milioni kutoka katika mgawo wa Sh1.62
bilioni zinazohusishwa na fedha zilizochotwa Akaunti ya Tegeta Escrow,
itajulikana Machi 29, wakati Bodi ya Rufaa za Kodi (Trab) itakapotoa uamuzi.
Tarehe hiyo imepangwa
na Makamu Mwenyekiti wa Trab, Hakimu Agusta Mmbando baada ya kukamilika kwa
hatua ya usikilizwaji pande zote mbili kwenye kesi hiyo.
Profesa Tibaijuka
alikata rufaa Trab baada ya TRA kumpelekea madai ya malipo ya kodi ya Sh586
milioni kutokana na mgawo wa Sh1.62 bilioni anazodaiwa kupokea kutokana na
fedha zilizochotwa kutoka akaunti hiyo iliyofunguliwa na Shirika la Umeme
(Tanesco) na kampuni ya kufua nishati hiyo ya IPTL kwa ajili ya kuhifadhi fedha
za malipo ya ununuzi wa umeme wakati mzozo wao ukiwa mahakamani, lakini
zikachotwa kwa njia ambayo ilizua shaka.
Rufaa hiyo
ilisikilizwa na Hakimu Mmbando Februari 17, 19 na 22 wakati Profesa Tibaijuka
alipokuwa akitoa ushahidi.
Inadaiwa kuwa Profesa
Tibaijuka, ambaye aliondolewa katika wadhifa wake wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kutokana na sakata hilo, aliwekewa fedha hizo kwenye
akaunti yake na James Rugemalira, Mkurugenzi wa VIP Engineering & Marketing
Limited iliyokuwa kati ya wanahisa wa IPTL.
Kutokana na mgawo huo,
Desemba 31, 2015, TRA ilimtaka alipe kodi hiyo, baada ya kushindwa kufanya
marejesho kutokana na mgawo huo.
Hata hivyo, alipinga
madai hayo na kisha akakata rufaa Trab kupinga hatua ya TRA kumtaka alipe kiasi
hicho cha kodi, pamoja na mambo mengine akidai kuwa hajawahi kupokea fedha hizo
kutoka kwa Rugemalira.
Katika rufaa hiyo
namba 22 ya mwaka 2015, Profesa Tibaijuka anadai kuwa makadirio hayo ya TRA ya
malipo ya kodi ni kinyume cha Sheria ya Kodi na hakupaswa kufanya marejesho kwa
kuwa hakupokea kipato chochote katika muda huo uliotajwa.
Akiongozwa na wakili
wake, Dk Nshalla Rugemeleza wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, Profesa
Tibaijuka alidai kuwa fedha hizo zilikuwa ni mchango uliotolewa kwa Taasisi ya
Joha Trust, kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Barbro Johansson inayomilikiwa
na taasisi hiyo.
Profesa Tibaijuka
alidai kuwa yeye si mwanahisa wa taasisi hiyo, bali ni mmoja wa wadhamini na
kwamba TRA ilipuuza ushahidi wake kuwa VIP ilitoa mchango kwa Joha Trust na
yeye kama mdhamini alizipeleka Joha Trust kupitia Bank M.
Aliongeza kuwa TRA
haikuzingatia ukweli kwamba Joha Trust na yeye ni vitu viwili tofauti, huku
akisisitiza kwamba fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya Joha.
Hata hivyo, wakili wa
TRA, Noah Tito ilipinga madai ya Profesa Tibaijuka akidai kuwa utetezi wake
hauna msingi kwani fedha hizo ziliingia kwenye akaunti binafsi ya Profesa
Tibaijuka na siyo ya Joha Trust.
No comments:
Post a Comment