Watu watano wamefariki
dunia na wengine watano kujeruhiwa, baada ya nyumba waliyokuwa wakiishi
kuangukiwa na kifusi na mti wakiwa wamelala, ajali hiyo ilisababishwa na
kupasuka kwa karo la majitaka la nyumba ya jirani iliyo juu ya mlima.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kinondoni, Christopher Fuime alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa
karo hilo na kwamba maji yaliyotoka kwa kasi yaling’oa mti, kifu
si na kisha kuifunika
nyumba ya jirani iliyojengwa bondeni na kusababisha vifo hivyo.
Alisema tukio hilo
lilitokea jana alfajiri katika Mtaa wa Ukwamani Kata ya Kawe jijini Dar es
Salaam, na waliokufa ni Ephraim Manguli (47), watoto wake Daniel Ephraim (5) na
Frederick Ephraim (1). Wengine ni mjukuu wa mwenye nyumba hiyo, Greyson
Clarence (3) pamoja na msichana wa kazi za ndani aliyetambulika kwa jina moja
la Maria.
“Majeruhi ni pamoja na Emilia Nakiete (19) aliyejeruhiwa mkono wa kulia
na kidevu na Fadhili Fariji (8) aliyejeruhiwa mguu wa kulia. Wengine watatu
walitibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala na kuruhusiwa. Majeruhi wawili bado
wamelazwa na miili ya marehemu imehifadhiwa hospitalini hapo,” alisema Kamanda Fuime.
Baada ya kutafutwa,
mmiliki wa nyumba hiyo Blandina Clarence Akilizao (49), alisema nyumba yake
ilikuwa na wapangaji sita wenye familia, huku familia yake ikiwa na watu saba.
“Ndani ya nyumba
nilikuwa na watoto wawili, wadogo zangu wawili na wajukuu wawili, pia kulikuwa
na familia tano zilizokuwa na watu 17 jumla,” alisema mama huyo kwa uchungu.
Blandina alisema nyumba
hiyo aliachiwa na mumewe aliyefariki dunia mwaka 2000 na kwamba hivi sasa hana
msaada wowote, kwani akiba ya fedha aliyokuwa nayo kiasi cha Sh200,000
imefukiwa na kifusi na hajui namna ya kuipata.
Mmoja wa mashuhuda wa
tukio hilo ambaye ni mpangaji, Msafiri Nyamolelo alisema ajali hiyo ilitokea
ghafla na kabla ya ukuta kuanguka, ulisikika mlipuko na baadaye kelele za maji,
kisha kishindo kikubwa juu ya paa.
“Karo lilipasuka na kwa kuwa ardhi hiyo hapo
juu kwa muda mrefu ni dampo lenye mifuko mingi, ardhi ilikuwa imeoza, hivyo
miti mikubwa ambayo iliota huko iling’oka baada ya karo kupasuka na kutua juu
ya paa la nyumba sambamba na udongo kutoka juu nao ukafunika,”alisimulia Nyamolelo.
Akizungumzia tukio
hilo, Katibu Mtendaji wa Mtaa wa Ukwamani, Kata ya Kawe Kassim Mbezi alisema
chanzo cha ajali ni kupasuka kwa karo la choo na maji yaliyomwagika ambayo
yaliuzoa mti huo na kifusi kilisombwa na kuifunika nyumba hiyo.
“Tulipofika eneo la tukio tuliwakimbiza majeruhi wote Mwananyamala,
lakini kwa bahati mbaya walifariki baada ya kufika mapokezi wote walitoka
wakiwa bado wanahema, lakini ilipofika saa tatu asubuhi tukaambiwa kwamba
kulikuwa na ‘house girl’ hivyo baada ya kufukuafukua tukaupata mkono na baadaye
kuufikia mwili mzima, huyu tulimtoa akiwa tayari amefariki,” alisema Mbezi.
Mbezi alitoa wito kwa
wakazi wa bonde hilo kuhama kwa kuwa gema bado linaonekana na ni hatari na
changamoto kubwa ni namna ya kukabiliana na maafa kabla ya kutokea.
No comments:
Post a Comment