Walimu wa shule ya msingi Isabilo wilaya na Mkoa wa Geita wamegoma kufanya kazi tangu Januari 25 mwaka huu kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kukosa morali ya kazi baada ya wanakijiji kuvamia na kuwapiga walimu wawili kwa tuhuma za kuwaadhibu watoto wao.
Wakizungumza na Storm habari wakati wa ziara ya Katibu wa Chama cha walimu C.W.T tawi la Geita Mwl. John Kafimbi walimu waliofanyiwa kitendo hicho Medard Zacharia na Deograsi Ristone wamesema kitendo kilichofanywa na wananchi kuwapiga walimu kimewafedhehesha sana.
Kaimu mkuu wa shule ya msingi Isabilo mwl. Athuman Augustine amesema sababu ya kuadhibiwa kwa wanafunzi ni kutokana na kutokufika shuleni hali ambayo iliwapelekea kuwapa adhabu ya viboko vitatu kwa kila mwanafunzi ambaye hakuhudhuria siku ya usafi shuleni wakati wa likizo.
Katibu wa Chama cha Walimu Wilayani Geita John Kafimbi amesema kuwa suala hilo halitavumiliwa kuona walimu wanadhalilishwa na kwamba hatua kali zichukuliwe na Serikali dhidi ya wananchi ambao wametenda kitendo hicho.
Pia imeelezwa kuwa wakati walimu hao wakitoa adhabu mmoja wa wanafunzi hao anayesumbuliwa na mapepo alianguka na kuzimia hali iliyopelekea wazazi kuwa na jazba kisha kuhamasisha wananchi kuvamia shuleni hapo.
No comments:
Post a Comment