Hali ya kisiasa
visiwani Zanzibar, inazidi kuwa tete huku siasa za visasi, chuki na uhasama
zikionekana kurejea kwa kasi, hali hiyo imejitokeza baada ya ofisi za matawi
matano ya Chama cha Wananchi (CUF) zilizopo Pemba na moja Unguja kuchomwa
moto na watu wasiojulikana.
Matukio ya kuchomwa
moto kwa ofisi hizo yamekuja siku mbili baada ya watu wasiojulikana kuchoma
moto maskani ya CCM ya Sauti ya Kisonge iliyopo mjini Unguja.
Hata hivyo Jeshi la
Polisi visiwani humo limetangaza kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini watu
waliohusika na matukio hayo.
Uchomaji huo
ulifanyika usiku wa kuamkia jana saa 8 usiku, ambapo watu hao walichoma moto na
kuteketeza nyaraka za chama hicho.
Matawi yaliyochomwa
moto ni Kilimahewa mjini Unguja Wilaya ya Magharibi, Mkanyageni, Kiwapwa, Kiuyu
Minungwini, Wingwi na Kinowe yote ya Kisiwani Pemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir, amethibitisha kutokeo kwa matukio hayo.
Amesema kutokana na
hali hiyo tayari ameagiza askari wake kuanza uchunguzi wa tukio hilo haraka ili
waliohusika watiwe nguvuni na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“Ni kweli kuna hilo tukio ingawa kwa sasa nipo
safari kuelekea Unguja na tayari nimeagiza kuanza kwa uchunguzi wa matukio haya
ili wahusika waweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
“…siwezi kusema kama matukio haya yana
uhusiano wa masuala ya kisiasa ingawa huu ni uhalifu kama uhalifu mwingine,” alisema Kamanda Nassir.
Akizungumzia tukio
hilo, Mbunge wa Wingwi, Juma Kombo Hamad (CUF), alilaani tukio hilo huku
akiwatuhumu wafuasi wa CCM kuhusika nalo.
Alisema hatua ya CUF
kutangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka
huu imekuwa ikiwaumiza CCM.
“Haya mambo yapo wazi tumeumizwa vya kutosha
lakini katika hilo mimi binafsi wala sifichi hapa kuna mkono wa CCM na
sisi hatutarudi nyuma tunaendelea na msimamo wa chama,” alisema Hamad.
Kauli ya Maalim Seif
Machi 4, mwaka huu,
Akizungumza na wafuasi wake waliomtembelea nyumbani kwake, Katibu Mkuu wa
CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, alisema yuko tayari kukamatwa kutokana na
msimamo wake wa kutotambua uchaguzi wa marudio.
“Msidhani kuwa mtatupiga shavu la kulia tukawageuzia la kushoto. Kila
mara tunaibiwa, tunapigwa, tunafanywa kila kitu. Tukisema kuwa watu wajilinde,
inakuwa nongwa.
“…basi tunawaambia kuwa kuitwa polisi, kuwekwa
ndani, kufunguliwa mashtaka ya bandia, hata kuteswa, hayo ni mambo yamekuwa
yakitutokea tangu 1992 tumeshayazoea,” alisema Maalim Seif.
Alisema udhalilishwaji
kama huo haujawahi kukirudisha nyuma chama chake, zaidi ya kukiongezea
umashuhuri na ufuasi mkubwa visiwani Zanzibar, huku akilituhumu Jeshi la Polisi
kwa kuwa ‘tawi la CCM’ ambalo litakuwa dhamana wa machafuko yoyote
yatakayotokea.
Katika hatua nyengine,
Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais katika Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka
jana alirudia msimamo wa chama chake wa kutoshiriki kile alichodai
uchaguzi wa marudio ulioitishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (ZEC), Jecha
Salim Jecha, Machi 20, mwaka huu.
Alisema yeye
alishashiriki uchaguzi na kushinda na hahusiki kabisa na uchaguzi mwengine. “Ninamwambia Jecha kuwa uchaguzi huo ni
wenu peke yenu,” alisema Maalim Seif.
No comments:
Post a Comment