Ni tiba inayoleta
mapinduzi ya vita dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa sababu sindano moja
itakuwa mbadala wa kumeza vidonge vya mwezi au zaidi.
Ni kweli kwamba kwa sasa
hakuna dawa inayoweza kuponyesha Ukimwi, lakini kuna dawa za kupunguza makali
na kutibu athari zinazotokana na maambukizi ya virusi vyake.
Kwa muda mrefu sasa, watu
wenye maambukizi ya virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini na wale
wanaougua maradhi nyemelezi, wamekuwa wakitumia vidonge kukabiliana na tatizo
hilo.
Kwa sasa matibabu ya
Ukimwi kwa kutumia vidonge yanawalazimisha watumiaji wa dawa hizi kumeza aina
tatu za dawa au zaidi kila siku.
Ingawa utaalamu wa
kuunganisha dawa zaidi ya moja umepunguza mzigo wa kumeza idadi kubwa ya
vidonge, lakini suala la kumeza dawa kila siku bado ni changamoto katika
matibabu ya Ukimwi.
Miongoni mwa changamoto
kubwa zinazoambatana na kumeza vidonge kila siku ni pamoja na kusahau,
kushindwa kumeza dawa kutokana na maudhi ya dawa, kukwepa hali ya unyanyapaa au
kushindwa kumeza pale mgonjwa anapokabiliwa na tatizo la kutapika.
Hali hii mbali na kuwa
mzigo kwa wagonjwa, lakini pia inaathiri ufuasi mzuri wa dawa kwa baadhi ya
watu.
Ni ukweli usiopingika
kuwa, ufuasi mbaya na matumizi ya dawa za ARV yasiyozingatia kanuni na
maelekezo sahihi ya wataalamu wa tiba kwa sababu yoyote ile, yanaambatana na
hatari ya kusababisha usugu wa virusi vya Ukimwi dhidi ya dawa.
Lakini pia, hali hii
inachangia wagonjwa wengi kushindwa kupata nafuu hata kama wanaendelea na
matibabu.
Wanasayansi kwa muda
mrefu sasa, wamekuwa wakitafuta njia mbadala ya kupunguza idadi ya vidonge au
kuachana na matibabu ya kumeza kila siku.
Utafiti wa hivi karibuni
unaonyesha kuwa katika siku za usoni, matibabu ya Ukimwi hayatategemea tena
umezaji wa vidonge kila siku na badala yake wagonjwa wataanza kutumia dawa kwa
njia ya sindano.
Sindano za ARV
zitapunguza au kuondosha changamoto na hofu ya watu kushindwa au kusahau dozi
ya kila siku ya ARV. Sindano hizi kwa mujibu wa watafiti zitakuwa zinatolewa
mara moja kwa mwezi au kila baada ya miezi mitatu.
Wanasayansi wa kampuni ya
kutengeneza dawa ya GlaxoSmithKline ya Marekani kwa kushirikiana na wale wa
kampuni ya Janssen ya Ubeligiji, mwaka 2013 aliripoti kuwa hatua ya kwanza na
ya pili ya majaribio ya dawa za ARV kwa njia ya sindano kwa binadamu,
yameonyesha mafanikio na usalama mkubwa. Watafiti wa maswala ya dawa za ARV
katika kitivo cha Afya ya Jamii cha Chuo Kikuu cha Columbia Marekani, nao
wanakiri kuwa ARV za sindano zina uwezo mkubwa wa kukabiliana na VVU.
Kwa sasa kampuni za ViiV
Healthcare na Janssen yanaendelea na mikakati ya kufanya majaribio ya dawa hizi
katika hatua ya tatu ya majaribio. kampuni hizo zinatazamia kuanza majaribio ya
hatua ya tatu mwaka huu.
Wataalamu wa maswala ya
utabibu wanaamini kuwa hii itakuwa hatua muhimu katika jitihada za kuboresha
tiba ya Ukimwi duniani.
Hata hivyo, wataalamu
wanadai kuwa, watu watakaotumia ARV za sindano ni wale ambao watakuwa wametumia
kwanza dawa za vidonge na kupunguza kwa kiwango kikubwa wingi wa virusi katika
damu yao.
Dk Dominique Limet ambaye
ni mkurugenzi wa kampuni ya ViiV Healthcare, anasema: “Ikiwa jaribio hili
litafanikiwa, watu wenye maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ambao kiwango cha
virusi ndani ya damu yao ni cha chini, watapata njia mbadala ya kutumia
sindano.”
Wataalamu pia wanasema
kuwa, ARV za sindano zinaweza kuwa na manufaa pale zitakapotumika kama kinga
kwa watu walioko kwenye mazingira yanayoongeza hatari ya maambukizi ya VVU,
ikiwa ni pamoja na wanandoa wenye hali tofauti za maambukizi.
Kutokana na ukweli kwamba
ARV za sindano zinalenga watu ambao wametumia kwanza vidonge na kudhibiti
virusi kwa ufanisi, wagonjwa ambao ufuatiliaji wa matibabu yao si mzuri, kwa
maana ya kutotumia dawa kikamilifu, wanaweza kushindwa kufaidika na maendeleo
ya kisayansi ya ugunduzi mpya wa njia ya kutumia ARV za sindano.
Uzuri wa ARV kwa njia ya
sindano ni kwamba haina usumbufu na maudhi mengi ikilinganishwa na kumeza
vidonge kila siku.
Pamoja na mafanikio haya
ya kisayansi katika tiba ya Ukimwi, baadhi ya wanasayansi wana wasiwasi kuhusu
ufanisi wa tiba hii hasa linapokuja swala la mtu kupata mzio wa dawa.
Dk Paul E. Sax, profesa
wa maswala ya tiba katika Chuo Kikuu cha Harvard anasema kuwa, kama itatokea
mtu akaanzishiwa dawa hii ya sindano ambayo inakaa mwilini kwa zaidi ya mwezi
na ikamsababishia madhara kama vile mzio, dawa hii itasababisha mateso makubwa
kwa mgonjwa.
Wachunguzi wengine wa
mambo wanadai kuwa, madhara mengine ya ARV za sindano yanaweza kuwa ni kutokea
kwa usugu wa virusi dhidi ya dawa kwa watu ambao watashindwa kupata dozi kwa
wakati kama wanavyopangiwa.
Hata hivyo wataalamu
wengi wanaamini kuwa ARV za sindano zinazotolewa mara moja kila mwezi au mara
moja kila baada ya miezi mitatu, zitapunguza kwa kiwango kikubwa changamoto na
adha kwa watu ambao walikuwa wanapata maudhi kwa kumeza vidonge vingi kila
siku.
Wengi wanaamini kuwa njia
hii ya kutumia dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, itasaidia kwa
kiwango kikubwa idadi ya watu wanaoshindwa kufuatilia na kutumia vizuri dawa
zao na itaboresha maisha ya wagonjwa wengi wenye tatizo la upungufu wa kinga
mwilini.
No comments:
Post a Comment