Tuesday 23 February 2016

SERIKALI KUWEZESHA UMEME VIJIJINI IFIKAPO 2025.



Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr.John Pombe Magufuli imedhamilia ifikapo mwaka 2025 vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme.
Hayo yamesemwa na naibu waziri wa nishati na madini Dk.Medard Kalemani alipokuwa akizungumza na wananchi katika kijiji cha kachwamba kata ya kachwamba na ilemela  wilayani Chato mkoani Geita.

Dr.Kalemani  amesema kwamba mradi wa umeme unaotekelezwa na wakala wa nishati vijijini REA utakuwa na gharama  nafuu hivyo kila mtanzania atumie fursa hiyo kujiletea maendeleo yeye mwenyewe.

Ameongeza kuwa miaka miwili ijayo vijiji vyote vya jimbo la Chato vitakuwa tayari vimeunganishiwa umeme.
Aidha kwa upande wa madiwani wa kata ya kachwamba na ilemela  Stella Kimanunga na Thobias Ntagwanamba  wamemweleza Naibu Waziri  Kalemani changamoto zinazowakabili katika kata zao, kama mbunge mwenye dhamana ndani ya jimbo la chato.

Akijibu kero hizo Dk. Kalemani amesema zipo changamoto ambazo ameanza kuzichukulia hatua na nyingine ataziwasilisha kwa mawaziri wengine wenye dhamana ili ziweze kutatuliwa.

Naibu Waziri huyo wa nishati na madini yupo mkoani Geita kwa ziara ya siku tatu, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake aliyoianza mkoani Tabora, Kigoma  na sasa Geita, kukagua na kuwasha umeme katika vijiji vilivyofikiwa na nishati hiyo.

No comments:

Post a Comment