Rais waJamhuri ya muungano wa Tanzania Dr John Pombe Magufuli |
Siku 15 alizotoa Rais John Magufuli kwa wakuu wa mikoa,
wawe wamejumlisha wafanyakazi wote na kuhakikisha wanaondoa wafanyakazi hewa,
zimetimia leo. Baadhi ya mikoa imeanika idadi ya watumishi hewa, waliobainika
kupitia uhakiki huo, lakini mingi haijafanya hivyo.
Agizo hilo la Rais Magufuli ni sehemu ya maagizo kadhaa
aliyotoa Machi 15 mwaka huu wakati akiwaapisha wakuu hao wa mikoa jijini Dar es
Salaam; ambao aliwasisitiza kuwa ili mradi wamekubali kushika wadhifa huo,
wameingia kwenye mtego.
Pamoja na majukumu mengine waliyopewa kuhakikisha
wanayatekeleza katika uongozi wao, suala la watumishi hewa ni mtego
unaowakabili wakuu hao wa mikoa wakipaswa kujinasua nao ndani ya wiki hii ambao
siku zilizotolewa zimefika ukomo; Vinginevyo, wataweka rehani nyadhifa zao.
Majukumu mengine ambayo wakuu hao wa mikoa walipewa na
Rais wahakikishe wanayatekeleza, ni pamoja na kukabili ujambazi hususan wakuu
wa mikoa ya pembezoni inayokabiliwa na tatizo la utekaji magari kiasi cha
serikali kuamua kuweka utaratibu wa polisi kuyasindikiza.
Mengine ni kukabili watu wazembe, watendaji
wanaowanyanyasa wananchi, njaa, kodi za mazao, migogoro ya ardhi na kuhakikisha
wanasimamia mpango wa elimu bure unafanikiwa.
Tangu Rais atoe maelekezo hayo ya kukabili wafanyakazi
hewa, mikoa mbalimbali inaendelea na mchakato wa kuhakiki wafanyakazi kwenye
idara na taasisi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuwataka watumishi kuwasilisha
nyaraka mbalimbali ikiwemo barua za ajira.
Katika mchakato huo ambao umezaa matunda kwa kubaini
watumishi hewa waliokuwa wakilipwa mishahara, baadhi ya halmashauri
zililazimika kufuta huku baadhi ya halmashauri zimeamuru watumishi wake walio
masomoni na kwenye likizo, warudi mara moja katika vituo vyao vya kazi
kuhakikiwa.
Madudu yaibuliwa Miongoni mwa mikoa ambayo imetoa
taarifa za uhakiki ni pamoja na mkoa wa Dodoma, ambao umetajwa kuwa na
watumishi hewa 144. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, ameagiza
kupelekewa orodha ya watumishi hao na wakati huo huo kupatiwa maelezo kwa nini
kuna watumishi hewa na kutaka kupatiwa orodha za watumishi hao.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya
ofisi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa aliyehamia Mkoa wa
Songwe, Rugimbana alisema uhakiki wa watumishi wa serikali umebaini uwepo wa
idadi hiyo ya watumishi hewa .
Mkoa wa Kigoma pia ni miongoni mwa mikoa ambayo taarifa
zake za uhakiki zimeshatolewa ambako imebainika kuwapo watumishi hewa 169 kwa
kipindi cha mwaka uliopita.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Emanuel Maganga
amewataka wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote waliopo katika halmashauri zote
kutaja kiasi cha fedha kilichotumika kulipa mishahara watumishi hewa hao 169
ndani ya kipindi hicho cha mwaka mmoja uliopita.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huo wa Kigoma, watumishi
hewa waliowabaini, wamo waliokwishafukuzwa, waliofariki na wengine wasiokuwa na
sifa za kuwa watumishi wa umma.
Maganga ametaka fedha walizokuwa wakilipwa watumishi
hao hewa kwa ajili ya mishahara, zirudi na wakati huo huo wakurugenzi wawafute
kwenye orodha ya malipo.
Halmashauri za mkoa wa Kigoma zenye watumishi hewa na
idadi yake kwenye mabano ni Kasulu (78), Kigoma (23), Manispaa ya Kigoma Ujiji
(29), Buhigwe (11), Uvinza (19), Kibondo (5) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa yenye
watumishi hewa wanne.
Halmashauri ya Kakonko ndiyo pekee isiyo na mtumishi
hewa. Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili jana, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,
Evarist Ndikilo, alisema leo ambayo ndiyo ukomo wa muda aliotoa Rais, atatoa
taarifa kamili ya kazi hiyo ya kuhakiki wafanyakazi na kuondoa wafanyakazi hewa
watakaokuwa wamebainika.
Ndikilo alisema, ipo timu inayo endelea kufanya uhakiki
kwenye wilaya mbalimbali kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri. Likizo
zaahirishwa Kwa upande wa mkoa wa Dar es Salaam, Halmashauri ya wilaya ya
Temeke ililazimika kuwaita watumishi wake walioko masomoni na likizo kurudi
mara moja katika vituo vyao vya kazi wahakikiwe.
Msemaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Joyce
Nsumba alisema hivi karibuni uhakiki uliendelea kwa makundi mbalimbali wakiwemo
watumishi kutoka Idara ya Afya, Elimu, Fedha na Biashara, Kilimo, Mifugo,
Ujenzi na Maendeleo ya Jamii.
Wakati anazungumza na mwandishi wa habari hizi hivi
karibuni, Nsumba alisema walishahakiki watumishi 8,000. Sababu za uhakiki
Uamuzi wa Rais Magufuli kuamuru ufanyike uhakiki, ulitokana na uchunguzi
uliofanywa katika mikoa ya Singida na Dodoma katika halmashauri 14 na
kugundulika kwa watumishi hewa 202 wanaolipwa mishahara.
Aliagiza uhakiki kwa watumishi wote katika wizara,
mikoa, wilaya, idara,taasisi na Wakala za Serikali ndani ya siku 15. “Sasa
niwaombe ndugu zangu wakuu wa mikoa, najua mtakwenda kuwapa maagizo wakurugenzi
na wakuu wa wilaya.
Lakini niwape muda, ndani ya siku 15, wawe wamejumlisha
wafanyakazi wote, wamewatoa wafanyakazi hewa,” ali waagiza. Rais Magufuli
alisema mshahara ujao, ikigundulika kuwapo wafanyakazi hewa kwenye orodha ya
malipo, mkurugenzi husika ajihesabu hana kazi na atafikishwa mahakamani.
Vile vile amewaambia mawaziri, hususan Waziri wa Fedha
na Mipango aliyekuwapo kwenye hafla hiyo, wakawaeleze watendaji kwenye wizara
zao na taasisi mbalimbali wahakikishe wanawaondoa wafanyakazi hewa ndani ya
siku 15 na wasipotimiza agizo hilo hatua zitakuwa ni zilezile kwani sheria ni
msumeno.
Alisema inasikitisha kuona fedha zinazokusanywa
haziendi kwenye miradi inayopangwa, badala yake sehemu kubwa inatumika kulipa
mishahara ikiwemo hewa. Alisema kwa ujumla Serikali inalipa mishahara kila
mwezi kwa watumishi wake wa umma jumla ya Sh bilioni 549 mpaka bilioni 550.
Alisema kwa hali ilivyo, fedha nyingi zinaishia kwenye
mishahara feki. Nawapa Ma-RC siku 15 mhakikishe Wakurugenzi wa halmashauri zote
wamejumlisha idadi ya wafanyakazi wote waliopo na kuondoa wafanyakazi hewa
katika halmashauri zao,” alisisitiza Rais Magufuli.
Mikoa ya Tanzania Bara ni: Arusha, Dar es Salaam,
Dodoma, Tanga, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa,
Katavi, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Singida, Tabora,
Pwani, Manyara, Mara, Morogoro na Kilimanjaro
No comments:
Post a Comment