Mkuu
wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo amewasimamisha kazi madaktari wawili na
wauguzi watano wa Hospitali ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kutokana na uzembe
unaodaiwa kusababisha kifo cha mama mzazi Pendo Masanja na watoto wake mapacha.
Tukio hilo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya mapacha
wengine kupoteza maisha wakati wa kuzaliwa katika hospitali ya wilaya ya
nyamagana iliyopo Butimba jijini Mwanza kwa kile kinachoelezwa kuwa ni uzembe
wa wauguzi pamoja na madaktari wa hospitali hiyo kushindwa kumhudumia kwa
wakati mama mjamzito Suzan John machi 3 mwaka huu.
Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza pia amewasimamisha kazi wauguzi
wengine wawili wa hospitali ya Butimba ambao ni Nathan Bagaya na Edina
Mwesiga,Daktari mmoja wa Hospitali hiyo Furaha Kingunge na dereva wa gari la
kubeba wagonjwa ( AMBULANCE) Ghalib Hamad, huku akitangaza kuunda tume ya watu
wanne ikiongozwa na mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk. Onesmo Rwakyendera kwa
ajili ya kuanza uchunguzi dhidi ya watumishi hao.
Tume iliyoundwa na mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza kuchunguza uzembe
wa madaktari pamoja na watumishi wa hospitali hizo mbili za butimba na Sekou
Toure, huenda ikaja na majawabu sahihi na ufumbuzi wa changamoto zinazopelekea
kutokea kwa vifo vya watoto wachanga na akinamama wajawazito wakati wa
kujifungua.
No comments:
Post a Comment