Saturday, 5 March 2016

UMEKATA TAMAA? UNAHISI HUJIAMINI? FUATA HATUA HIZI KUMI USONGE MBELE.

  • Acha kujitahidi kumfurahisha kila mtu, Kumbuka kila mtu ana namna yake yake ya kufikiri ambayo ni tofauti kabisa na mwingine. Anza kwa kumfurahisha yule mtu uliyenae kila siku (AMBAE NI WEWE)… Ukifanikiwa kuwa na furaha juu yako mwenyewe, ni mlango wa mengine mengi mazuri. Jifunze kusema hapana hasa unapoona jambo halikuletei faida yoyote, itakuchukua muda lakini ndio njia bora ya kujifunza kujiamini.
  • Usiweke mafanikio yako mikononi mwa mtu mwingine, epuka maneno kama “akifanikiwa yeye na mimi ntafanikiwa”, “Ningekuwa na wazazi nisingeishi hivi” au “Ndoto zangu zote zimekufa baada ya fulani kufariki/kufukuzwa kazi/kufungwa/kuugua nk” Kumbuka alizaliwa ashiriki nafasi yake na sio yako. Amka Fanya Kazi.
  • Usisikilize muziki utakao kufanya ukose furaha, au kukukumbusha  maumivu au nyakati ngumu/mbaya za nyuma.
  • Unapotakiwa kuchagua njia moja kati ya mbili, Wakati Mwingine jifunze kuchagua njia ngumu. Hakuna “shortcut” kwenye mafanikio, hata wanaotangaza kuwa wana njia za haraka kukupa mafanikio/pesa na vingine, Kwa upande wao, wewe ndio njia yao ndefu ya kupatia mafanikio. EPUKA KUFANYWA MTAJI (hakuna vitu vya bure maishani)
  • Usisubiri Mafanikio Makubwa ndio Ufurahie Maisha! anza taratibu kwa kufurahia mafanikio yako jiulize ni maeneo gani kwenye maisha yako yamekaa sawa au ni eneo gani unahisi una uwezo mkubwa? anza kuyafurahia kwani hakuna wakati utakao kuwa sawa kwa asilimia 100 katika maisha yako yote.
  • Usiwe Mtu wa kuomba sana ruhusa kabla ya kufanya kitu. Cha msingi ni kuwaza ni nini utafanya ukizuiliwa au kukutana na changamoto mbele ya safari.
  • Unatakiwa ujue kwamba sio kila muda utakwenda na wakati, unapaswa kuyaacha mengine yaende kwani nayo yatapitwa na wakati. Isikupe shida kwa kuwa hauko kama wengine kwa kipindi fulani, jipe moyo kwani vitu vinapita ndani ya muda mfupi (hasa ulimwengu huu wa sayansi na teknolojia.
  • Usijiwekee sheria ambazo ni ngumu kuzifuata kwani utaishia kukata tamaa mapema na kuhisi maisha ni magumu.
  • Usijione hujafanikiwa na kukata tamaa kwa kujilinganisha na wengine ambao pengine ni wa umri wako kwani siku zote utahisi wana vitu bora zaidi yako, hwana majukumu mengi zaidi yako, wanakipato kikubwa kuliko wewe na hawana changamoto kama ulizonazo. Jambo la msingi ni kuelewa kuwa kila mtu anapigana vita dhidi yake mwenyewe, ana malengo yake, na hatuwezi kufanana fikra vinginevyo dunia nzima wote tungekuwa madaktari/walimu/waigizaji nk!
  • Usiache linalowezekana leo lifanyike kesho kwa kuhisi kesho itakuwa na ahueni. jambo la msingi ni kuhakikisha hauruhusu akili yako isimame kwani katika maisha kuna uelekeo wa aina  mbili tu… kwenda mbele au kurudi nyuma, unaposimama maana yake unarudi nyuma.

No comments:

Post a Comment