Waziri mkuu Kassim Majaliwa akitambulisha mfumo mpya wa malipo.
Serikali imeanzisha
mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao
unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
Hayo yamesemwa na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza
na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu alisema
mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote
nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa
Waziri Mkuu alisema
mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa
wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa
kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.
Kabla ya kuanzishwa
kwa mfumo huo, maafisa utumishi walipaswa kukusanya taarifa za watumishi wote
walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili
zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka HAZINA kwa maandalizi ya mishahara.
Akitolea mfano wa kada
ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa zinaanzia Idara ya
Utumishi wa Walimu (TSD) lakini anapaswa aende kuripoti kwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ambaye ni mwajiri wake chini ya
TAMISEMI.
"Hii ilileta ugumu wa malipo ya
kupanda madaraja, uhamisho ama likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo
fedha."
"Sasa hivi tuna Tume ya Utumishi wa
Walimu (TSC) ambayo iko chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa
hiyo ni rahisi wao kukaa pamoja na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote
hao wakalipwa bila bila kuchelewa," alisema.
Alisema mfumo huo umeanza
kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya za walimu na hadi sasa
umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi mshahara wake hata kama
ameajiriwa ndani ya mwezi huohuo.
"Kama mtumishi anaripoti kwenye kituo
kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi amefika na barua zake zote na ziko
sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa zake na wakati huohuo taarifa zitaonekana
Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na pia zitapokelewa kwa maafisa
wanaoshughikia mishahara kule HAZINA."
Alisema changamoto
pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa ni kutoingizwa taarifa
za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi husika.
"Hii ni kwa sababu matayarisho ya
mishahara yanakuwa yameshaanza. Kwa hiyo wengi walishauriwa kuripoti kati ya
tarehe 25 hadi tarehe 9 ya mwezi uliofuata na wote hawa hawakupata matatizo ya
kucheleweshewa mshahara," alisema.
Akifafanua kuhusu
upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa
utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa
daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika
marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa
watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa)
ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya
kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua hiyo hiyo " alisema
AKATISHA ZIARA
KUTOKANA NA MSIBA.
Wakati huohuo, Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amelazimika kukatisha ziara ya mkoa wa Simiyu ambayo
ilikuwa imalizike kesho kutokana na msiba wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri
ya Wilaya ya Maswa ambayo alipangiwa kuitembelea leo.
Mkurugenzi huyo Bw.
Traceas Kagenzi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kutokana na shinikizo la
damu. Atasafirishwa kwenda Muleba kwa mazishi.
Akitoa salamu za
rambirambi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Kagenzi iliyofanyika nyumbani
kwake Maswa mjini, Waziri Mkuu alisema ameshtushwa na msiba huo uliotokea
ghafla na kwamba Taifa limempoteza mtumishi mahiri ambaye bado Taifa lilikuwa
likimtegemea.
"Nimeshtushwa sana na taarifa za msiba huu.
Nimeambiwa hadi juzi usiku alikuwa akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hii kuandika
taarifa ya ziara ya wilaya hii. Kwa niaba ya Serikali, ninawapa pole sana
wafiwa na Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,"alisema.
"Nimelazimika kukatisha ziara ya mkoa huu
kwa sababu huyu ni mtumishi mwenzetu" alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 6, 2016.
No comments:
Post a Comment