Watu
wawili wamefariki dunia na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa baada ya basi la
kampuni ya Ndenjela linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Dar es Salaam
kuligonga kwa nyuma basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo ni daladala
linalofanya safari zake kati ya Igawilo na stendi kuu jijini Mbeya katika eneo
la Uyole, kwenye barabara kuu ya Tanzania - Zambia.
Ajali
hiyo imetokea majira ya alfajiri wakati basi la kampuni ya Ndejela likitokea
gereji kwenda katika kituo kikuu cha mabasi jijini Mbeya kwa ajili ya kuchukua
abiria ili kuanza safari ya kwenda Dar es Salaam, lakini lilipofika eneo la
Kilimo katika bonde la Uyole, ndipo basi dogo aina ya toyota Hiace ambalo
lilikuwa limesimama kituoni,likaingia ghafla barabarani na ndipo lilipogongwa
na kwa nyuma na basi hilo la Ndenjela ambalo lilikuwa kwenye mwendo mkali na
kusababisha daladala hilo kuacha njia na kugonga jiwe kubwa kando ya barabara.
Afisa
muuguzi msaidizi wa zamu katika hospitali ya rufaa Mbeya,Abdul Kumwambe
amethibitisha kuwepo kwa vifo vya watu wawili pamoja na majeruhi 13 ambao
wanatokana na ajali hiyo.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Mbeya,Kamishna msaidizi mwandamizi wa jeshi la polisi,Ahamed
Msangi amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi wa basi la kampuni
ya Ndenjela huku akidai kuwa uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.
No comments:
Post a Comment