Waziri mkuu Kassim Majaliwa amesema atawatuma mawaziri watatu
waje mkoa wa Simiyu ili wakae na uongozi wa kila wilaya pamoja na wananchi ili
kubaini tatizo la mipaka baina ya wilaya hizo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kauli hiyo imetolewa jana(Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati
akizungumza na mamia ya wakazi wa vijiji vya Mwakaluba na Mwandoya akiwa kwenye
siku ya tano ya ziara yake mkoani Simiyu.
“Tangu niingie hapa mkoani malalamiko ya mipaka nimeyapokea kila mahali
nilikopita. Nimeamua kuwatuma mawaziri watatu ambao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi; Waziri wa Maliasili ua Utalii,
Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Bw. George
Simbachawene waje mkoa huu kutatua matatizo yenu,” alisema.
“…Nitawatuma waje na wapite kila wilaya, wakae na kuzungumza na
wakulima na wafugaji ili kubaini ni chanzo cha tatizo la migogoro hii kwenye
mipaka ya vijiji na hifadhi ya Serengeti. Pia Waziri wa TAMISEMI itabidi atoe
ufafanuzi kuhusu agizo lao la kutofanya shughuli yoyote mita 60 kutoka kwenye
mto Simiyu ili wananchi waelewe,” alisema.
Mapema, Mbunge wa Kisesa ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi (OMR
– Mazingira) alimweleza waziri Mkuu mbele ya wananchi hao kwamba limetolewa
zuio linalowakata wakazi wa mkoa huo wasifanye shughuli zozote umbali wa mita
60 kutoka kwenye kingo za mto huo.
“Limebandikwa tangazo linalokataza wananchi waishio kando ya mto
Simiyu wasifanye chochote kuanzia Julai 30, 2016. Wananchi hawajashirikishwa
wala kuelezwa chochote zaidi ya kuona bango la matangazo tu. Watu wananakatazwa
wasichote maji wala kunywesha mifugo wakati hakuna mabwawa, itawezekanaje?
Tunaomba kauli yako kuhusu jambo hili,” aliongeza.
Ili kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi hapa nchini, Waziri
Mkuu alisema Serikali ina mpango wa kuunda mabaraza ya ardhi 100 kwa nchi nzima
ambayo yatakuwa na jukumu la kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati.
Akitoa taarifa ya wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw.
Erasto Sima alisema wilaya hiyo iliyoanzishwa Julai mosi, 1987 ina ukubwa wa
kilometa za mraba 8,835 ambapo asilimia 49 (sawa na kilometa za mraba 4,329) ya
eneo lote la wilaya hiyo ni hifadhi za wanyamapori.
Alilitaja eneo hilo kuwa ni pori la akiba la Maswa, sehemu ya hifadhi
ya Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na pori la hifadhi ya usimamizi
wa wanyama (WMA) la Makao na kwamba asilimia 51 iliyobakia indiyo inayotumiwa
kwa makazi ya watu, kilimo na malisho ya mifugo.
No comments:
Post a Comment