Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Baraka Konisaga,
amemwamuru Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adam Mgoyi kuwasimamisha kazi
madaktari wawili na wauguzi wanne katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana
iliyopo Kata ya Butimba kwa kushindwa kumuhudumia mama mjamzito aliyefikishwa
hospitalini hapo na kusababisha kujifungua watoto mapacha na baadaye kufariki.
Hatua hiyo imesababishwa na tukio la mgonjwa Suzana John (27)
mkazi wa Kata ya Mkolani kufikishwa na ndugu zake katika Hospitali hiyo,
aliyekuwa mjamzito na kupokelewa na Dk Norin Magesa na Muuguzi, Janet Foya
waliokuwa zamu ya usiku siku ya Machi Mosi, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku
na kushindwa kumuhudumia zaidi ya kutoa lugha isiyoridhisha, pamoja na uzembe.
Akielezea tukio hilo, mwanamke huyo ( Suzan John ) alidai kuwa
alianza kusikia uchungu na kuomba msaada kutoka kwa madaktari na wahudumu wa
afya waliokuwa hospitalini hapo bila mafanikio.
“Nilifika nikiwa hoi,
nikawaambia muda wangu tayari lakini hawakunisaidia zaidi ya kunitolea
maneno machafu.
"Wakati muda
ukizidi kwenda huku nikiwa sipewi huduma yoyote, nilihisi kubanwa
haja ndogo hivyo nikaamua kwenda chooni .
Kule chooni mambo
yakabadilika ghafla, mtoto wa kwanza akawa keshaanza kutoka.Bahati nzuri mle
chooni kulikuwa na beseni
"Nililichukua
lile beseni kwa ajili ya kuwaweka watoto huku niwakaita manesi.Manesi hao
walikuja wakanichungulia halafu wakarudi. Akaja Nesi mmoja mwanafunzi, akakata
kitovu akawaweka kwenye nguo, wakawa wamefariki,” Bi. Suzan alieleza kwa uchungu huku akilia.
Baada ya mapacha hao kufariki, ndugu wa mwanamke huyo
pamoja na wagonjwa wengine walioshuhudia mkasa huo walipandwa na hasira huku
wakitaka kuwapiga wauguzi hao.
Taarifa za vurugu hizo zilimfikia DC Konisaga ambaye alifika
hospitalini hapo na kukutana kwa dharula na Mkurugenzi wa Jiji, Adamu
Mgoyi, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana,
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa, Uongozi wa Hospitali na baadhi ya ndugu wa mgonjwa
Suzana John aliyejifungua watoto mapach.
Katika kikao hicho cha dharura, walipokea maelezo ya pande
mbili, kutoka kwa wauguzi na familia ya mgonjwa Suzana, na kupitia taarifa
zilizokuwa zimeandikwa na Madaktari wawili waliomuona mgonjwa huyo, ndipo DC
Konisaga akamuagiza Mkurugenzi Mgoyi na Kaimu Mganga Mkuu kuwasimamisha kazi
madaktari wawili na wauguzi wanne ili kupisha uchunguzi wa kitaalamu juu ya
tukio hilo.
Konisaga aliwataja wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Dk
Magesa na muuguzi Foya waliompokea mgonjwa wakiwa zamu ya usiku wa Machi Mosi,
mwaka huu na kushindwa kumpatia huduma zaidi ya kumtolea lugha chafu na uzembe
huku wakishindwa kutoa maelezo wakati wa kukabidhi majukumu kwa madaktari na
wauguzi walioingia zamu ya asubuhi ya Machi 2, mwaka huu.
DC Konisaga pia alieleza kuwa pamoja na kuingia kwa madaktari na
wauguzi wa zamu ya asubuhi ya Machi 2, bado hawakumjali na kumhudumia mgonjwa
huyo huku baadhi wakitoa lugha zisizo za faraja kwa ndugu wa mgonjwa.
Hata alipozidiwa na kupewa taarifa na ndugu wa mgonjwa huyo,
hawakufika na mara kadhaa walikuwa wakifika na kutoka bila kumudumia pamoja na
kumsikiliza akilalamika.
Aliwataja wengine wanaotakiwa kusimamishwa kazi mara moja ni Dk
Emiliana Mvungi, wauguzi ni Maria Mkankule, Suzana Sindano na Bibiana Moshi
ambao walikuwa zamu na kutomhudumia mgonjwa ambaye alijifungua katika mazingira
hatarishi akiwa Hospitalini hapo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo
amemwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Rweyendela Onesmo ambaye ni
Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure kupewa maelezo ya
kina kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Nangi William na Mganga
Mkuu wa Jiji, Dk John Andrew juu ya kushindwa kuchukua hatua pamoja na kupewa
taarifa hizo.
Mulongo pia amemuagiza Dk Onesmo kuunda tume ya uchunguzi
itakayoshughulikia suala la tukio hilo na kisha kukamilisha kazi hiyo kwa siku
moja na kumpatia taarifa ili hatua kali za maadili ya utumishi wa umma zichukue
mkondo wake ili pia kuwezesha kusaidia jinsi ya kuboresha utendaji wa kitaalamu
na kitabibu katika hospitali hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa
na wananchi kutokuwa na huduma nzuri kwa wagonjwa.
No comments:
Post a Comment