Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bweya katika Kijiji cha Bweya mkoani
Geita, Augustine Katemi (42) ameuawa baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na
mke wa mtu vichakani.
Mwenyekiti huyo alifariki dunia papohapo baada ya kudaiwa
kushambuliwa kwa sime na mume wa mwanamke huyo, mkazi wa Kijiji cha Luchili,
Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza.
Tukio hilo lilitokea saa nne usiku Machi 28 baada ya marehemu
kudaiwa kukutwa akifanya tendo la ndoa na Chausiku Isangula (32).
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Geita, Latson Mpojoli alisema hana za taarifa za tukio hilo na
kuahidi kufuatilia.
Ilielezwa kuwa Katemi aliuawa baada ya kushambuliwa kwa sime na
kufa papohapo na baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia mkewe kwa
kutumia sime hiyohiyo na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za
mwili na amelazwa kwenye Kituo cha Afya cha Nzera.
Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Bweya, Samson Walwa alisema
baada ya kutokea tukio hilo wananchi waliendesha msako na kumtia mbaroni
mtuhumiwa wakati akijaribu kutoroka kuelekea Sengerema.
Walwa alisema mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwa Edward Iswalala
alipokuwa amefikia kwa siri kutoka Luchili ili kufuatilia mwenendo wa mkewe
ambaye anadaiwa kuwa awali alimuaga kuwa anakwenda kumsalimia baba yake mzazi
anayetibiwa kwa mganga wa kienyeji.
“Inavyosemekana
alikuwa akifuatilia mienendo ya mke wake… sisi tulipomkamata tumemkabidhi Kituo
cha Polisi cha Nzera pamoja na nguo za marehemu (mwenyekiti) na zile za mkewe
kwani alipofanya mauaji hayo alizichukua nguzo zao hadi tulipomkata nazo,” alisema Walwa.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo, Jumanne Tole
alisema, Chausiku alimuaga mumewe kuwa alikuwa anakwenda kijiji cha Kalebezo
kumsalimia baba yake mzazi kwa waganga wa tiba asilia alikokuwa anatibiwa
lakini baada ya kufika na kumsalimia, alikwenda kwa kaka yake aitwaye
Ndagabwene Isangula huko Bweya alikofikwa na mkasa huo.
Alisema kuna madai kuwa mtuhumiwa alifika kijijini hapo kwa siri
akiwa amevaa nguo na kofia zilizochakaa ili asifahamike wakati akifuatilia
nyendo za marehemu na mkewe na akafanikiwa ikidaiwa kwamba alikuwa na watu
ambao walikuwa wakimpatia taarifa hizo.
No comments:
Post a Comment