Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda amezindua vitambulisho
vitakavyotumiwa na walimu kupanda daladala bure wakati wakitoka nyumbani kwenda
kazini.
Katika hatua nyingine Makonda ameziomba sekta mbalimbali nchini
kushiriki katika kutoa mawazo yao ya maendeleo ili taifa lisonge mbele badala ya
kuwa watazamaji.
Makonda aliyasema hayo Dar es Salaam jana mbele ya wazazi na
walimu wa Shule ya Sekondari ya Turiani wakati akizindua vitambulisho hivyo
vitakavyotumiwa na walimu wa wilaya yake kupanda daladala bure kufuatia mpango
aliouanzisha wiki iliyopita wa kuwasaidia walimu hao.
"Nawaomba watanzania na sekta mbalimbali kuwa na mawazo ya
maendeleo ambayo yatawekwa mezani na kuyafanyia kazi jambo litakalo msaidia
Rais wetu Dk.John Magufuli katika kuliinua taifa kiuchumi badala ya kumuachia
kila kitu akifanye yeye" alisema Makonda.
Makonda alitoa mwito kwa makondakta wa daladala kutoa
ushirikiano kwa walimu hao kesho wakati watakapoanza kupanda magari yao huku
wakijua walimu ndio waliowafundisha na kufikia hatua hiyo ya kazi walizonazo.
Ofisa Elimu wa Sekondari wa Wilaya hiyo, Rogers Shemwelekwa
aliwaomba wananchi hao na walimu kuendelea kuunga mkono jitihada za Makonda za
kuwaletea maendeleo na kumuombea kwa mungu badala ya kumbeza kwani kazi hizo
anazozifanya ni kwa ajili ya wananchi.
No comments:
Post a Comment