Tuesday 5 June 2018

KINARA WA UTEKAJI AUWAWA MKOANI GEITA



Mtu mmoja anayejulikana kwa majina ya Panda Kinasa mwenye miaka 36 anayetuhumiwa kuwa kinara wa utekaji  watu ameuwawa kwa kupigwa na risasi makalioni wakati akijaribu kuwatoroka polisi baada ya kuwapeleka kwenye mashimo alikokuwa ametupa miili ya watu wawili wilayani Bukombe Mkoani Geita.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Geita Mponjoli Mwabulambo amesema tukio la kwanza limetokea tarehe 24 mwezi wa 3 ambapo kijana Leornad Samwel mwenye miaka 18 alitekwa majira ya saa saba usiku.

Amesema mwanamke Nkwimba Mwandu alitekwa majira kama hayo na kwamba watekaji walitoa namba za simu wakitaka watumiwe fedha za kumkomboa vinginevyo wanawaua watu hao.

Kamanda Mponjoli amesema mtuhumiwa huyo alimpiga kikumbo askari kwa lengo la kutoroka na walipojaribu kumpiga risasi ili kumuogopesha hakuwa tayari kusimama ndipo askari wakampiga risasi kwenye makalio na kisha akafariki akiwa hospitalini.

Katika tukio jingine Kamanda Mponjoli amesema unyang’anyi wa kutumia silaha ulifanyika June 3 mwaka huu ambapo watu wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na fimbo, mapanga na bunduki ambayo haijafahamika aina yake walivamia maduka mawili ya vifaa mbalimbali na kupora hata hivyo jeshi la polisi lilifanikiwa kuwatia nguvuni na majeruhi wanaendelea vizuri kwa sasa.

No comments:

Post a Comment