Walimu wanane wa Shule ya Sekondari Mihama, Kata ya Kitangili, Wilaya ya
Ilemela Mkoani Mwanza, wamesimamishwa kazi, watano kati yao wakishikiliwa na
polisi kwa tuhuma za kufanya mapenzi na wanafunzi.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa
Mwanza, Magesa Mulongo aliyetembelea shule hiyo jana,pia amevunja bodi ya shule
hiyo baada ya kubainika kutofanya kikao hata kimoja tangu ilipoteuliwa Aprili
24, 2013.
Pamoja na Mkuu wa
Shule, Joseph Malifedha, walimu wengine waliotiwa mbaroni jana ni Rodrick
Uroki, Denis Sanga, Edmund Boaz, Steven Samuel.
Walimu watatu
waliokuwa wakifundisha shuleni hapo, lakini wakahamishwa na hivi sasa wanasakwa
na polisi kwa tuhuma hizo ni Joseph Lamongi na Joeza Mzava waliohamia Sekondari
ya Sangabuye pamoja na Abdallah Mtelwe aliyehamia Tanga.
Malifedha anadaiwa
kuwachangisha fedha wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu kwa ajili ya
picha za kuweka kwenye vitambulisho (passport size).
Akitangaza uamuzi huo,
Mulongo alisema tume maalumu ya uchunguzi iliyoundwa Januari 27, kuchunguza
tuhuma dhidi ya walimu hao kujihusisha na mapenzi na wanafunzi imebaini ukweli
baada ya kuwahoji wanafunzi kadhaa.
“Ni fedheha na haivumiliki kuona walimu
wakifanya mapenzi na wanafunzi wao. OCD wakamate walimu wote na uanze uchunguzi
mara moja na kukusanya ushahidi utakaowezesha wahusika kufikishwa mahakamani
ili sheria ichukue mkondo wake,” aliagiza Mulongo.
Amri hiyo ilitekelezwa
mara moja kwa walimu hao kuwekwa chini ya ulinzi.
Mulongo pia alimwagiza
Katibu wa Idara ya Utumishi wa Walimu Mkoa wa Mwanza, Genzi Sahani kuwaandikia
barua za onyo walimu wa kike shuleni hapo kwa kushindwa kulinda na kutetea
masilahi ya wanafunzi wa kike waliokuwa wakidhulumiwa kingono na walimu wenzao kiasi
cha baadhi yao kuathirika kisaikolojia.
Pia, alimwagiza Ofisa
Elimu Mkoa wa Mwanza, Khamisi Maulid kuangalia uwezekano wa kuwahamishia shule
nyingine wanafunzi waliodhulumiwa kingono na walimu wao ili kuwaepusha na
matatizo ya kisaikolojia.
Maulidi alisema
wanafunzi walioathirika zaidi ni wale wa kidato cha nne.
Katibu wa Chama cha
Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Mwanza, Said Mselem alisema kitendo hicho
kimeifedhehesha taaluma ya ualimu na kuahidi kuwa ofisi yake itatanua wigo wa
uchunguzi hadi kwenye shule nyingine.
No comments:
Post a Comment