Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa mtu kwanza kutekeleza
agizo la Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam la kuhakiki silaha, ambapo bunduki zake
mbili aina ya Shortgun na Pistol zimehakikiwa nyumbani kwake Ikulu Jijini Dar
es salaam.
Uhakiki huo umefanywa na maafisa wa Jeshi la Polisi wakiongozwa na Kamanda wa
Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam, Kamishna Simon Sirro.
Akizungumza baada ya
kukamilika kwa zoezi hilo, Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es
salaam na Jeshi la Polisi kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa Silaha, na ametoa
wito kwa watu wote wanaomiliki silaha nchi nzima kuhakikisha zinahakikiwa.
Dkt. Magufuli pia
amelitaka Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kukabiliana na watu wanaojihusisha
na vitendo vya uharifu ili kutokomeza kabisa vitendo hivyo.
"Ni aibu kumuona askari polisi mwenye
silaha ananyang'anywa silaha, ni aibu, na nasema hiyo ni aibu, mpaka jambazi
akunyang'anye silaha na wewe una silaha?" Amehoji Rais Magufuli
Kwa upande wake
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es salaam Kamishna Simon Sirro,
amemshukuru Rais Magufuli kwa kuunga mkono zoezi hilo na amesema Jeshi la
Polisi limejipanga kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.
Katika hatua nyingine,
Rais Magufuli ametaka pande zinazogombea kiti cha Umeya katika Jiji la Dar es
salaam, kukamilisha mchakato wa kumpata Meya katika uchaguzi uliopangwa
kufanyika kesho tarehe 22 Machi, 2016 badala ya kuendelea kurumbana.
Dkt. Magufuli amesema
upande wowote uwe tayari kupokea matokeo ya uchaguzi huo, ili Meya apatikane na
Jiji liweze kuendelea na mipango yake ya kuwahudumia wananchi bila vikwazo.
"Mahali tunapostahili kushinda kama tumeshinda tushinde kweli, lakini
mahali tunaposhindwa napo tukubali kushindwa, na hiyo ndio demokrasia ya
kweli" ameongeza Raisi.
No comments:
Post a Comment