Mkurugenzi wa Sensa ya
Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim
Kwesigabo akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari(hawapo
pichani) kuhusu mfumko wa bei wa Taifa leo Jijini Dar es Salaam, Mfumuko wa bei
umeshuka toka asilimia 3.8 mwezi Aprili hadi kufikia 3.6 Mei. Kushoto ni Meneja
wa Ajira na Bei toka NBS, Ruth Minja.
Ofisi ya Taifa ya
Takwimu (NBS) leo imetoa taarifa ya mfumuko wa bei kwa mwezi Mei mwaka huu
ambao umepungua hadi kufikia asilimia 3.6 ikilinganishwa na asilimia 3.8
ilivyokuwa kwa mwezi Aprili mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Sensa ya
Watu na Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ephraim
Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa bei kumechangiwa sana na kupungua kwa
mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula.
“ Baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia
kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mahindi kwa asilimia 10.3, unga wa
mahindi kwa asilimia 12.5, mtama kwa asilimia 13.8, unga wa mihogo kwa asilimia
15.2, viazi mviringo kwa asilimia 9.0 na mihogo mibichi kwa asilimia 12.6,
alisema bwana Kwesigabo.
Aidha ameongeza kuwa kasi ya mabadiliko ya bei
za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018 imepungua
ikilinganishwa na kasi ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2018.
Hali ya mfumuko wa bei kwa baadhi ya nchi za
Afrika Mashariki kwa mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018 nchini Uganda umepungua
hadi asilimia 1.7 kutoka asilimia 1.8 kwa mwaka ulioishia mwezi aprili 2018.
Aidha kwa upande wa Kenya mfumuko wa bei kwa
mwaka ulioishia mwezi Mei, 2018 umeongezeka kidogo hadi asilimia 3.95 kutoka
asilimia 3.73 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili, 2018.
Mfumuko wa bei unapima kiwango cha kasi ya
mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi.
No comments:
Post a Comment