Siku ya Figo Duniani huadhimishwa duniani kote kila
Alhamisi ya pili ya mwezi Machi tangu mwaka 2006. Mwaka huu itaadhimishwa leo
tarehe 10/3/2016.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya
Figo mwaka 2016 ni “Chukua Hatua Mapema Kuepuka Magonjwa ya Figo kwa Watoto”.
Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo ya figo yanayoikabili
jamii yetu hususani watoto.
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine
duniani inaadhimisha siku hii.
Wizara Kwa kushirikiana na Chama
cha Watalaam wa Magonjwa ya Figo Tanzania kutoa elimu ya kujikinga na madhara
ya magonjwa ya figo kwa kuzingatia kanuni za afya na kupima mapema ili kutambua
na kupata matibabu kwa wakati.
Magonjwa ya figo huathiri utendaji
wa viungo hivi muhimu katika mwili wa binadamu, miongoni mwa kazi za figo
mwilini ni kutengeneza kemikali inayochochea utengenezaji wa chembe nyekundu za
damu, kusaidia upatikanaji wa madini yanayoimarisha mifupa, kusaidia
upatikanaji wa vitamin D mwilini, kurekebisha shinikizo la damu na kuondoa
maji, uchafu utokanao na utendaji wa mwili na sumu mwilini. Magonjwa ya figo
huathiri watu mbalimbali katika jamii bila kujali umri, kuanzia watoto wachanga
mpaka wazee.
Magonjwa ya figo hutokana na sababu
mbalimbali kulingana na umri wa waathirika. Magonjwa haya kwa watoto
husababishwa na magonjwa mengine yakiwemo malaria, kichocho, homa ya manjano,
kuhara, ugonjwa wa kisukari kwa watoto na maambukizi ya bakteria ya koo na
ngozi. Pia yapo magonjwa yanayotokana na matatizo ya mfumo wa mkojo ambayo
watoto huzaliwa nayo.
Zipo sumu na dawa za mbalimbali
zinazoathiri figo ikiwa ni pamoja na dawa za maumivu kama diclofenac hasa
zinapotumika kiholela. Matumizi ya mitishamba yameripotiwa kuathiri utendaji wa
figo.
Kwa watu wazima chanzo kikubwa cha
magonjwa ya figo ni ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu. Pia utumiaji wa
dawa, mitishamba na magonjwa ya kuambukiza kama ilivyo kwa watoto yanaweza
kuathiri figo kwa watu wazima. Yapo pia magonjwa mengi ambayo huathiri figo
moja kwa moja mfano mawe ya figo na njia ya mkojo.
Tafiti za ugonjwa wa figo
zinaonyesha kuwa kati ya mwezi Agosti 2014 na Februari 2015 kati ya watoto 513
waliopimwa magonjwa ya figo katika Hospitali za Bugando na Sekou Toure asilimia
16.2% walikuwa na matatizo ya figo. Katika utafiti huo ilionekana watoto
waliokuwa na magonjwa ya figo walikuwa na malaria, ugonjwa wa seli mundu
(sickle cell anaemia) maambukizi ya bakteria kwenye koo na ngozi na kutumia
mitishamba kabla ya kufika Hospitali. Utafiti huu unaonyesha wazi uwepo wa
matatizo ya figo kwa watoto.
Utafiti mwingine uliofanyika Mkoani
Kilimanjaro kati ya mwezi Januari na Juni 2014, uliohusisha watu 481 kutoka
katika kaya 146, asilimia 7% walionekana kuwa na matatizo ya figo. Utafiti huu
ulionyesha uhusiano wa karibu kati ya uwepo wa tatizo la figo na ugonjwa wa
kisukari, shinikizo la damu na matumizi ya mitishamba.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku
ya figo duniani kwa mwaka 2016, inalenga kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu
kinga dhidi ya ugonjwa wa figo kwa watoto. Jamii inawahamasishwa kuchukua hatua
kuwahi Hospitali pale tunapohisi mtoto anaweza kuwa na ugonjwa unaoweza
kusababisha matatizo ya figo.
Pia ni muhimu kwa wananchi wote
kuchukua hatua ya kupima ili kujua kama wana matatizo ya figo.
Pia ni muhimu kwa wananchi wote
kuchukua hatua ya kupima ili kujua kama wana matatizo ya figo hasa wale wenye
matatizo yanayosababisha matatizo ya figo hususani kisukari na shinikizo la
damu. Wizara inatoa wito kwa watoa huduma za afya kuhakikisha wanawapima
matatizo ya figo mara kwa mara wale wote wanaosumbuliwa na magonjwa
yanayoathiri figo yakiwemo kisukari na shinikizo la damu.
Pamoja na magonjwa yaliyoripotiwa
kusababisha matatizo ya figo, yapo mambo yanayochochea uwezekano wa kupata
magonjwa ya figo yakiwemo ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi,
mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji
wa sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo
wa mawazo.
Ili kuzuia magonjwa ya figo na
maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya ambazo ni
ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa kiasi
kikubwa kuzuia mtu kupata magonjwa yanayosababisha matatizo ya figo, na kwa
wagonjwa ambao wana magonjwa yanayoathiri figo kama kisukari na shinikizo la
damu ni vizuri wakazingatia ushauri wa wataalamu ama kutumia dawa kama
wanavyoelekezwa ili kuzuia uwezekano wa kupata matatizo ya figo.
Serikali inaendelea na utekelezaji
wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa magonjwa yasiyo ya
kuambukiza ikiwemo matatizo ya figo. Aidha, Serikali, Sekta Binafsi, Mashirika
ya Kimataifa na Taasisi zinazotoa huduma bila faida zinaendelea kuandaa na
kurekebisha Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa
magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutumia maadhimisho haya
kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.
Serikali inaendelea kuandaa
miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo magonjwa ya figo, kisukari na shinikizo la damu.
Serikali imeimarisha ushiriki wa wadau mbalimbali na inaendelea kuhimiza
Taasisi za Umma na za Binafsi kuweka mkazo ili kukabiliana na magonjwa yasiyo
ya kuambukiza.
Kwa kutambua gharama za kutibu
ugonjwa wa figo, Serikali imekuwa ikigharimia matibabu ya wagonjwa wenye
matatizo ya figo ikiwemo upandikizaji wa figo kwa wale wagonjwa ambao figo zao
zimeshindwa kufanya kazi kabisa.
Pia Serikali imejitahidi kusogeza
huduma za figo kwa wananchi kwa kuanzisha huduma za figo kwa Hospitali za Rufaa
baada ya kupeleka wataalamu wa magonjwa ya figo. Hospitali zenye wataalamu wa
magonjwa ya figo ni Hospitali ya Taifa Muhimbili, Hospitali ya KCMC, Hospitali
ya Rufaa Mbeya, Hospitali ya Bugando na Hospitali ya Benjamin William Mkapa
iliyopo Dodoma.
Mpaka sasa wagonjwa 190 wakiwemo
watoto wawili wamepata huduma ya kupandikizwa figo na wanapata huduma katika
kitengo cha figo Muhimbili na katika Hospitali nyingine za rufaa.
Pia Serikali imeweka mkakati wa
kuhakikisha huduma za upandikizaji wa figo zinapatikana hapa nchini haraka
iwezekanavyo ili kupunguza gharama za kupelekwa wagonjwa nje ya nchi na kutoa
huduma kwa watanzania wengi zaidi. Miongoni mwa mikakati iliyopo ni kuimarisha
huduma za figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa wataalamu nje
ya nchi kwa mafunzo ili kufanikisha upatikanaji wa hizo huduma hapa Tanzania.
Tanzania inaungana na Mataifa
mengine duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2011 la kuwa na
mpango kabambe wa kuthibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Lengo ni kuhakikisha
Mataifa yote duniani yanapunguza magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa asilimia 25
ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia lengo hili ni muhimu kushirikisha wadau wengi
zaidi na kufanya kazi kwa ushirikiano.
Wengi wetu wanaweza kuwa na
matatizo ya figo bila kujitambua hasa wale wenye magonjwa ya kisukari na
shinikizo la damu. Magonjwa ya figo yanaweza kuwa na dalili kadhaa zikiwemo
kuvimba mwili kunakoanzia usoni, kupungua au kukosa mkojo kabisa, kukojoa mkojo
wenye damu au rangi ya kahawia, kuwa na shinikizo la damu, kuchoka mwili na
kupungukiwa na damu. Dalili hizi hujitokeza baada ya figo kupata athari kubwa,
hivyo inawezekana kabisa mtu kuwa na tatizo la figo bila kuwa na dalili. Mara
unapoona una dalili nilizozitaja hapo juu ni vizuri ukaenda Hospitali ili
upimwe na wataalamu na kupata matibabu au ushauri.
Matatizo ya figo yakigundulika
mapema inawezekana kupata matibabu ambayo yatazuia uharibifu wa figo na
kumuwezesha mgonjwa kuishi bila kuhitaji matibabu makubwa ambayo ni ya gharama
kubwa ikiwemo kupandikizwa figo.
Hivyo Wizara inatoa wito kwa kila
mmoja wetu kuhakikisha kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza
usionyeshe dalili yoyote mapema.
Ni vyema kila mmoja akapima afya
yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya afya. Endapo mtu atatambuliwa kuwa
ana ugonjwa wa figo anashauriwa kutumia huduma za afya kulingana na ushauri
atakaopewa na wataalam wa afya.
Kwa wale ambao wameshajitambua kuwa
na matatizo ya figo, kisukari na shinikizo la damu lakini hawatumii huduma za
afya ipasavyo, wanaaswa kutumia huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao
na kuepusha athari zinazotokana na magonjwa hayo.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
10 Machi, 2016
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
10 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment