Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba amesema
uamuzi wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuondoka CCM, ulikuwa moja ya
sababu ya chama hicho tawala kushinda urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka
jana.
Makamba pia amemshauri
Lowassa kuachana na harakati za kuwania urais kwa kuwa ni muda mrefu tangu
alipogombea kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na kuishia kwenye uteuzi ndani ya
CCM.
“Kuondoka kwa Lowassa kwenda
upinzani ndiyo kulirahisisha sisi (CCM) kushinda uchaguzi kwa sababu
kuliwaondolea wapinzani hoja mbili muhimu ambazo ni ufisadi na mabadiliko,”
alisema Makamba, ambaye alikuwa msemaji wa kampeni za CCM kwenye Uchaguzi Mkuu
uliopita, wakati wa mahojiano ofisini kwake.
Lowassa, ambaye alikuwa
waziri mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne kabla ya kujiuzulu mwaka 2008
baada ya kuibuka kashfa ya Richmond, alijiengua CCM Julai 28, mwaka jana ikiwa
ni siku chache baada ya jina lake kuchujwa pamoja na wagombea wengine 33 wa
urais kwa tiketi ya CCM.
“Niliwekewa mizengwe
kuhakikisha jina langu halifiki Kamati Kuu na Halmashauri Kuu,” alisema Lowassa wakati akitangaza kujiengua CCM
na baadaye akajitetea kuwa kuhusishwa kwake kwenye sakata la Richmond
kulitokana na kupokea maagizo kutoka juu.
Akiwa Chadema, Lowassa
alipitishwa kugombea urais na akaungwa mkono na vyama vingine vitatu
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hali iliyomfanya aweke rekodi
ya upinzani tangu kurejeshwa kwa vyama vingi baada ya kuzoa asilimia 39.97 za
kura akizidiwa na John Magufuli wa CCM, ambaye alipata asilimia 58.4.
Katika mazungumzo na
Mwananchi, Makamba alikiri CCM kupata ushindani mkubwa kutoka vyama vya
upinzani katika uchaguzi huo uliokuwa na msisimko, lakini akasema kuhama kwa
Lowassa kuliwapa nguvu zaidi.
“Kuhusu Lowassa kujiunga na
upinzani kwamba ndio kuliwapa nguvu (Ukawa), hapana. Suala hili kwangu
nalitazama tofauti,” alisema Makamba.
“Mnapomchukua mtu (Lowassa) ambaye
miaka 10 iliyopita mmekuwa ndiyo mnashika picha yake kwamba ni kielelezo cha
rushwa na ufisadi ndani ya nchi na CCM, halafu mnamchukua, mnaenda naye kwenye
kampeni maana yake ile hoja (ya ufisadi) mmeamua kuiachia.”
Makamba pia alisema
Lowassa amekuwa sehemu ya mfumo wa utawala na uongozi wa nchi kwa miaka 40,
hivyo hawezi kuwa kinara wa mabadiliko.
Alisema kitendo cha
Chadema kuhubiri mabadiliko huku mgombea akiwa Lowassa, maana yake ni kwamba
wameamua kuiacha hoja hiyo.
“Kwa tathmini yangu na utafiti
tulioufanya, hizo hoja mbili ambazo siku zote zilikuwa silaha za upinzani, wameamua
kuziachia na matokeo yake ilikuwa rahisi kwetu (CCM) kupata ushindi,”
alisema.
Alipoulizwa atamwabia
Lowassa nini siku wakikutaka, Makamba alisema: “Kwanza, nimemsikia akisema
atagombea tena mwaka 2020, nitamwambia mambo mawili; hii habari kuwa aliibiwa
kura aachane nayo maana si kweli, pia inampunguzia heshima maana uchaguzi
umeisha na wananchi wameridhika lakini wewe peke yako unabaki kualalamika.”
Pili, alisema hoja ya
pili itakuwa ni kumshauri asigombee urais mwaka 2020 kwa kuwa CCM watamshinda
na atakuwa ametumia miaka 25 kuwania nafasi hiyo bila mafanikio.
“Alianza kuutaka urais
mwaka 1995 ni kipindi kirefu na mle bungeni tutakuwa na wabunge ambao
kabla hawajazaliwa, Lowassa alikuwa anagombea. Nadhani nchi hii watu wana
vipaji, waachiwe nafasi watoe mchango wao kwenye kujenga demokrasia ya nchi
yetu. Kifupi apumzike,”
alisema Makamba.
Katika uchaguzi wa mwaka
1995, Lowassa aliondolewa mapema kwenye mbio za urais kwa tiketi ya CCM na
mwaka 2005 hakuchukua fomu, badala yake akawa nguzo kuu ya kampeni za rafiki
yake, Jakaya Kikwete ambaye aliibuka kidedea CCM na baadaye kushinda urais.
Baada ya uchaguzi, Kikwete alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu.
Akizungumza na wazee wa
Chadema jimbo la Ubungo hivi karibuni, Lowassa aliwataka kutokata tamaa na kujipanga
kimkakati kujiandaa na kuimarisha chama kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2020 na
kuahidi kugombea tena.
Makamba pia alisema
alitegemea nguvu ya upinzani kuongezeka kadri muda unavyokwenda kwa sababu
baada ya zaidi ya miaka 23 tangu kurejeshwa kwa mfumo wa siasa za ushindani,
upinzani usingeendelea kubakia uleule.
Alisema hivi sasa mwamko
wa Watanzania katika kusikiliza mawazo na fikra tofauti umeongezeka na kwamba
CCM imepewa changamoto kutokana na mabadiliko ya mfumo katika jamii, uhuru
wa habari, wa kuamua na kujieleza.
“Yaliyotokea ni matokeo
ya mafaniko ya maendeleo ya demokrasia katika nchi yetu miaka 10 iliyopita,” alisema.
Alisema hali hiyo
imewafanya wananchi kutoogopa kujitokeza na kuunga mkono waziwazi upinzani,
akivituhumu baadhi ya vyombo vya habari kujipambanua msimamo wake kwa wagombea
wa upinzani.
Kwa nyakati tofauti
viongozi wa Chadema, wakiongozowa na mwenyekiti wao Freeman Mbowe wamenukuliwa
wakisema kuwa mambo yanayofanywa na Rais Magufuli ni mawazo ya wapinzani na
yapo katika ilani ya uchaguzi ya Chadema, lakini Makamba amepinga akisema
wanamsifia Rais ‘kwa mamna yake’.
“Nadhani wanajaribu kudandia treni
inayokwenda vizuri. Pengine ndiyo namna nzuri ya kiungwana ya kumsifia mtu kwa
sababu wamekosa ujasiri wa kusema anafanya kazi nzuri,” alisema
Makamba.
“Ilani yetu ukiisoma ina
vipaumbele vikubwa vinne; cha kwanza ni kupinga rushwa, uzembe na ubadhilifu wa
mali ya umma. Hatua zinazochukuliwa sasa ni ahadi tulizotoa katika ilani. Pili,
wakati wa kampeni Rais Magufuli aliahidi haya anayofanya. Tulitegemea
atayafanya kwa sababu aliyasema katika kampeni.”
Alisema CCM ilimteua
Magufuli kwa sababu ilijua inateua aina ya kiongozi atakayesaidia kutokana na
kujulikana kwa utendaji wake.
“Hiyo ilani ya Chadema
sisi hatuijui na hata mgombea wao alikuwa anaongea dakika tatu, sasa kwa muda
huo ataongea jambo gani la kuigwa,” alisema Makamba huku akieleza mambo mengine mawili yaliyokuwepo
kwenye ilani ya CCM kuwa ni ajira na umasikini.
No comments:
Post a Comment