Tarehe ya 23 Machi
kila mwaka Shirika la Hali ya Hewa Duniani(WMO) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
huadhimisha siku ya hali ya hewa Duniani. Maadhimisho haya ni kumbukumbu
ya siku ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani tarehe 23 Machi,1950.
Mamlaka ya Hali ya
Hewa Tanzania (TMA) ilianzishwa kwa sheria ya wakala wa serikali Na. 30 ya
mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi mwezi Desemba 1999. Mamlaka inafanya kazi zake
kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
na inaiwakilisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania katika Shirika hilo.
Tanzania kupitia (TMA) inaadhimisha siku hii
ya hali ya hewa duniani kwa kusherehekea mafanikio yaliyofikiwa na WMO tangu
kuanzishwa kwake na Mafanikio ya uboreshaji wa huduma za hali ya hewa hapa
nchini.
Miongoni mwa majukumu
ya TMA ni pamoja na kufanya shughuli za uangazi, kukusanya na kuhifadhi data
na takwimu za hali ya hewa, kutoa utabiri wa hali ya hewa na usambazaji wa
taarifa za hali ya hewa hapa nchini na nje ya nchi.
TMA pia inaiwakilisha
Tanzania katika masuala ya hali ya hewa kimataifa na pia
Mamlaka inashirikiana na wadau wengine hapa nchini na katika kanda ya
Afrika mashariki na kusini mwa Afrika ili kuboresha utabiri wa hali ya hewa wa
msimu ambao ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Tunaposherekea siku ya
hali ya hewa Duniani, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inajitahidi kutoa
huduma za hali ya hewa za kuaminika, zinazotolewa kwa wakati, zenye
viwango vya usahihi vinavyokubalika na katika lugha rahisi na ya
kueleweka ili kukidhi mahitaji ya jamii ikiwa ni pamoja na watoa maamuzi na
hivyo kuchangia katika maendeleo ya Taifa. Mfano mzuri wa matumizi ya taarifa
za hali ya hewa katika kufanya maamuzi ni katika sekta ya kilimo na
usafiri wa Anga.
Uelewa
wa kuanza, kuisha na urefu wa msimu wa mvua ni muhimu katika kufanya maamuzi ya
shughuli za kilimo kama vile, wakati gani wa kupanda na kuvuna, pia aina gani
ya mazao yanaweza kupandwa , wakati gani wa kunyunyizia dawa na namna gani ya
kuhifadhi mazao. Katika Usafiri wa anga taarifa za hali ya hewa ni
muhimu wakati wa kutua, kupaa na usafiri wa ndege inapokuwa angani. Aidha,
taarifa za hali ya hewa zinatumika kibiashara na wamiliki wa ndege katika kujua
kiasi cha mafuta yanayohitajika na kiasi cha mzigo unaoweza kubebwa katika
safari husika.
Maeneo
mengine ambayo taarifa za hali ya hewa ni za muhimu ni katika ujenzi, mipango
miji pamoja na utafiti na uchimbaji wa mafuta na gesi. Taarifa za
hali ya hewa husaidia wahandisi na maafisa mipango miji kuainisha maeneo ya
kuweka miundombinu mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya maji safi na maji
taka, ujenzi wa madaraja n.k. Takwimu za vimbunga na
mfumo wa upepo katika ukanda wa Pwani ni muhimu sana katika shughuli
zinazoendelea za utafiti na uchimbaji wa mafuta. Idadi ya siku ambazo mvua
itanyesha na hali ya joto ya mahali husika ni muhimu katika sekta ya utalii.
Taarifa
za matukio ya hali mbaya ya hewa kama vile mafuriko na ukame, upepo mkali
pamoja na mvua ya mawe na kujua eneo litakalo athirika ni muhimu sana katika mipango
mbalimbali ya maendeleo.
Hii ni baadhi ya
mifano michache tu ambapo uhitaji na uelewa wa huduma za hali ya hewa
hauepukiki. Katika kuhakikisha kuwa jamii yetu inafikiwa na huduma hizi muhimu
za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) husambaza taarifa hizi
kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kama vile,
Facebook, Twitter, YouTube.
Kutokana na kuongezeka
uelewa wa sayansi ya hali ya hewa, utabiri wa hali ya hewa umeendelea
kuongezeka viwango vya usahihi na hivyo nashauri sekta zote za kiuchumi na
kijamii hapa nchini kuendelea kutumia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na
Mamlaka ya hali ya hewa katika kupanga mipango yao ya muda mfupi na
mrefu.
Endapo utabiri wa hali ya hewa utolewao na TMA
utazingatiwa na kutumiwa kwa makini utasaidia sana katika kupunguza athari za
majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa Adha, ikumbukwe kwamba, kuna
uwezekano mkubwa wa kuokoa maisha na kupunguza hasara ya upotevu wa mali kwa
kuwa na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa.
TMA imepata cheti cha ubora cha
kimataifa (ISO 9001:2008) katika utoaji wa huduma bora za hali ya
hewa kwa usafiri wa anga. Cheti hiki kilipatikana mwaka 2011 na hii ni sifa kwa
nchi yetu hasa ikikumbukwa kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kupata cheti
hicho kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara. Mipango
iko mbioni kuhakikisha huduma zitolewazo na TMA katika sekta zote zinasajiliwa
na shirika la viwango duniani. Hivyo tunaposherehekea siku ya hali
ya hewa Duniani naendelea kuwashauri watanzania wenzangu katika sekta zote za
kiuchumi na kijamii kutumia taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu ya
taifa letu.
Nawatakia
maadhimisho mema ya siku ya hali ya hewa duniani mwaka huu wa 2016.
No comments:
Post a Comment