Wzairi wa ujenzi,Uchukuzi na mawasiliano Prof.Makame Mbalawa(Mwenye koti la bluu) akisikiliza maelezo ya wakandarasi.
Serikali imesema itachukua hatua kali kwa
kampuni ya Halotel kama itashindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wa
kusambaza huduma za simu na mtandao katika ofisi za Serikali katika kila Wilaya
nchini kote.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano
Prof. Makame Mbarawa wilayani Maswa wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Simiyu na kusisitiza kutoa ushirikiano
unaostahili kwa kampuni hiyo.
“Makubaliano yetu kati ya
Serikali na Halotel ni kuunganisha ofisi za Umma kwa mtandao zikiwemo shule
tatu katika kila Wilaya, Hospitali, Mahakama na Ofisi za Polisi ili kuwezesha
mkakati wa mawasiliano vijijini kutekelezeka”, alisema Prof. Mbarawa.
Aidha alieleza kuwa ifikapo mwaka 2017 kila eneo hapa nchini
litakuwa na huduma ya mawasiliano ya mtandao na kuwezesha wananchi wote
kunufaika na huduma hizo.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua Ujenzi wa Barabara
ya Lamadi-Bariadi KM 71.8 na Bariadi-Maswa KM 49.7 na kuwapongeza makandarasi
wanaojenga barabara hizo kwa kazi nzuri wanayofanya.
“Nawapongeza kwa kazi
nzuri mnayoifanya, hakikisheni kazi yenu inauwiana na thamani ya fedha na
kuhakikisheni wafanyakazi wazawa wanapewa kipaumbele katika kazi wanazoziweza
na kupewa mikataba stahiki ya kazi wanazozifanya”, alisititiza Prof. Mbarawa.
Waziri Prof. Mbarawa
amemuagiza mkandarasi anaejenga barabara ya Maswa-Mwigumbi KM 50.3 kuhakikisha
nyumba zinazojengwa kwa ajili ya mkandarasi zinajengwa kwa ubora ili zitumike
kwa muda mrefu.
“Nakuagiza Meneja wa
TANROADS, hakikisha nyumba hizi baada ya mradi wa barabara kukamilika
unazikabidhi kwa jeshi la polisi ili waweze kuzitumia kwa ajili ya makazi na
ofisi”,
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Eraston Mbwilo
alimtaka Waziri Prof. Mbarawa kuelekeza nguvu za ujenzi wa ofisi na nyumba za
watumishi katika mkoa huo.
Prof.Mbarawa akitoa maelezo flani kwa vibarua wa wanaofanya kazi katika mradi wa barabara ya Maswa-Mwigumbi Km 50.3,Mkoani Simiyu.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bi. Rosemary
Kirigini amemuomba Waziri Prof. Mbarawa kuwawezesha Wakala wa Majengo nchini
(TBA) kukamilisha mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo unaojengwa
sasa kwa miaka mitano ili kuipunguzia Wilaya hiyo adha ya kutumia jengo chakavu
ambalo si salama hasa kipindi cha mvua.
Prof. Mbarawa pia
amekagua Kiwanja wa Ndege kilichopo Mkoa wa Shinyanga na ofisi za Mamlaka ya
Hali ya Hewa (TMA) kiwanjani hapo na kusisitiza kuwa Serikali iko katika hatua
za kuboresha uwanja huo kuwa wa kisasa ili kuvutia mashirika mengi ya ndege
kutumiwa kiwanja hicho.
Waziri Prof. Mbarawa yupo kwenye ziara ya kukagua miradi ya
ujenzi kwenye sekta za barabara, nyumba, viwanja vya ndege na mkongo wa taifa
wa mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo ametembelea Wilaya za
Busega, Bariadi na Maswa mkoani Simiyu.
No comments:
Post a Comment