Wito umetolewa kwa
wafanyabiashara na wananchi wa Mkoa wa Geita kujitokeza kwa wingi katika
Kampeni Maalum ya Huduma na Elimu kwa Mlipakodi kwa ajili ya kuwasilisha
malalamiko, changamoto, maoni pamoja na kupata elimu ya masuala ya kodi na
ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwa ujumla.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo mkoani Geita, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Mhandisi Robert
Gabriel amesema kuwa, wafanyabishara na wananchi watumie fursa ya kampeni
hiyo itakayomalizika tarehe 13 Aprili, 2018 kupata elimu sahihi ya masuala ya
kodi na tozo mbalimbali.
“Nachukua fursa hii
kutoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wa mkoa huu hususani wale
wanaoishi katika maeneo ya Masumbwe, Ushirombo, Rulembela, Katoro, Lunzewe,
Namonge, Nyanghw’ale, Bwanga na Muganza kujitokeza kwa wingi ili waweze
kujifunza, kupata huduma na kutoa maoni yao kwa watalaam wetu wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kuyatolea ufafanuzi na kuyafanyia kazi,”
amesema Mhe. Luhumbi.
Nae Meneja wa TRA
mkoani hapa, James Jilala amesema kuwa, lengo kuu la kufanya kampeni hii
maalumu ni kuelimisha, kusikiliza malalamiko, changamoto pamoja na kupokea
mrejesho na maoni mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
“Kampeni hii ni
mwendelezo wa Wiki ya Elimu kwa Mlipakodi iliyofanyika nchi nzima kuanzia
tarehe 5 hadi 9 Machi, 2018 katika ngazi ya mkoa. Kutokana na matokeo ya
kampeni ile mkoani hapa, tumeona ni muhimu tuwe na kampeni nyingine maalumu
ambayo inafanyika maeneo mbalimbali katika wilaya zetu tofauti na ile ya kwanza
iliyofanyika Geita mjini tu,” amefafanua Jilala.
Kwa upande wake
kiongozi wa timu ya watalaam kutoka TRA Makao Makuu Maternus Mallya ameeleza
kuwa, timu yake imejipanga vizuri na tayari kazi imeanza kufanyika katika vituo
vyote vilivyotengwa kwa ajili ya kampeni hiyo.
“Hapa ninapozungumza,
wenzangu wako kwenye maeneo husika wanaendelea kufanya kazi. Hivyo, kama
alivyosema Mhe. Mkuu wa Mkoa, nami natoa rai kwa wananchi wote mkoani hapa,
kujitokeza kwa wingi ili waweze kukutana na watalaam wetu kwa ajili ya kupata
huduma na elimu ya mlipakodi,” amesema Mallya.
Kampeni Maalum ya
Huduma na Elimu kwa Mlipakodi mkoani Geita imeanza leo tarehe 9 hadi 13 Aprili,
2018 ambapo pamoja na mambo mengine, wafanyabiashara na wananchi watasajiliwa
na kupatiwa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) pamoja na kuelimishwa kuhusu
ulipaji wa Kodi ya Majengo kwa njia ya kieletroniki.
No comments:
Post a Comment