Waziri wa Nchi Ofisi (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye
Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimishi ya
Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Dunani wakati wa mkutano wake na
waandishi wa habari uliofanyika Bungeni Dodoma Aprili 25, 2018.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi.Khadija Mwenda akieleza jambo
wakati wa mkutano wao na waandishi wa habari uliohusu maandalizi ya maadhimishi
ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi Dunani Bungeni Dodoma, Aprili 25,
2018.
Baadhi wa waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Waziri wa
Nchi Ofisi (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama (hayupo pichani) wakati wa mkutano wake uliohusu maandalizi ya
maadhimishi ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi uliofanyika Bungeni
Dodoma Aprili 25, 2018.
Serikali imesema kuwa usalama mahali pa kazi ni
kichocheo cha ujenzi wa uchumi wa Viwanda hapa nchini ikiwa ni moja ya juhudi
za Serikali kuchochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa
habari leo mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali Pa
Kazi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Watu Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa dhamira ya Serikali
Kujenga uchumi wa Viwanda itatekelezeka kwa ufanisi kutokana na juhudi za
serikali katika kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanakuwa na mazingira salama
yakufanyia kazi kote nchini.
“Serikali haiwezi kutekeleza dhana ya Ujenzi wa
uchumi wa Viwanda pasipo usalama mahala pa kazi ndio maana inaweka mkazo katika
kuhakikisha kuwa mazingira ya kazi katika maeneo yote hapa nchini yanakuwa
salama ndio maana OSHA imekuwa ikiendelea kusimamia vyema jukumu hili.”
Alisisitiza Mhe. Mhagama
Akifafanua Mhe. Mhagama amesema kuwa suala la
usalama mahala pa kazi ni jukumu la kila mmoja na si, la Serikali peke yake
kama baadhi ya watu wanavyodhani.
Aliongeza kuwa watu 10,000 katika sekta isiyo
rasmi wamepatiwa mafunzo kuhusu usalama na afya mahala pa kazi hali
inayochochea maendeleo kwa kuongeza tija na kupunguza ajali zinazoweza
kuepukika au kuzuilika.
Tutaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa watu
wenye ulemavu hasa viziwi zaidi ya 300 watapatiwa mafunzo kuhusu Usalama mahala
pa kazi na afya ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kupitia OSHA kushirikisha
makundi yote katika kukuza na kuongeza tija katika uzalishaji.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa tuzo kwa
waajiri wanaozingatia Afya na Usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi wao hali
inayochochea ukuaji wa uchumi.
Siku ya Afya na Usalama mahali pa kazi
itaadhimishwa Kitaifa Mkoani Iringa tarehe 28/ 4/ 2018 ambapo Tanzania
itaungana na mataifa mengine kuadhimisha siku hiyo.
Pia Waziri Mhagama alitoa wito kwa waajiri wote
kujisajili OSHA ili watambulike na waweze kutoa taarifa zitakazosaidia
kuboresha hali na mazingira ya kufanyia kazi.
AWALI
OSHA ni Taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia
sheria Na. 5 ya Mwaka 2003 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi. Taasisi hii
inawajibu wa kufanya kaguzi za kiusalama sehemu zote za kazi Tanzania Bara,
kufanya Tafiti, Mafunzo na kuweka takwimu zote za usajili pamoja na taarifa za
ajali, Magonjwa na vifo vinavyotokana na mazingira hatarishi ya sehemu za kazi
na vile vile ndio Mshauri wa Serikali wa masuala yanayohusiana na Usalama na
Afya sehemu za kazi . Taasisi hii imekuwa ikifanikisha program mbalimbali
ikiwemo kutoa elimu.
(PICHA ZOTE NA OFISI YA
WAZIRI MKUU -DODOMA)
No comments:
Post a Comment