Waziri wa Menejimenti
ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika amesema kazi kubwa ya
usalama wa taifa ni kukusanya habari na kuishauri serikali na wala si kukamata
watu kwa mabavu.
Mkuchika ameyasema
hayo jana Aprili 16 bungeni wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala
wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha
2018/2019.
“Naomba nichukue
nafasi hii kufafanua sheria ya usalama wa taifa inasema nini, usipojua kazi za
idara ya usalama wa taifa, utawapa lawama kwa kazi ambazo si zao,” alisema.
Alisema idara hii
hutekeleza majukumu kulingana na sheria ya usalama wa taifa namba 15 ya mwaka
1996 na sheria hiyo katika kifungu cha nne, inasema kazi yake ni kukusanya,
kuchambua na kuishauri serikali hatua za kuchukua.
Alisema ameamua
kulisema hilo kwa kuwa wabunge wengi wamezungumzia kuhusu watu wa idara ya
usalama kukamata watu ovyo na kwa kutumia mabavu.
“Pili haitakuwa kazi
ya idara ya usalama, kumfuatilia fuatilia mhalifu. Nimeona niiseme hiyo kwa
sababu mazungumzo mengi yameelekeza huko, mtu ameuawa ni ‘polisi kesi’, hakuna
nchi ambayo idara ya usalama ina shughuli ya kukamata watu,” alisema.
Alisema: “Kama
mnataka usalama wa taifa wafanye kazi ya kukamata watu basi walilete suala hilo
bungeni.”
No comments:
Post a Comment