Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), inaratibu ziara ya viongozi wa makampuni ya biashara zaidi ya 30 kutoka Ufaransa ambao ni wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi ya Ufaransa (MEDEF) yenye mtandao wa makampuni zaidi ya 7100
Ziara hiyo itakayofanyika kuanzia tarehe 15 – 18 Aprili 2018, inalenga kukuza ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Ufaransa; kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini Tanzania; kushawishi makampuni makubwa ya Ufaransa kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo nishati, miundombinu, viwanda, maji n.k na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania na Ufaransa kubadilishana uzoefu na kuanzisha ushirikiano baina yao.
Ukiwa nchini, ujumbe huo utapata fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wakuu wa serikali na kushiriki katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Ufaransa litakalofanyika tarehe 18 Aprili 2018, jijini Dar es Salaam.
Aidha, baada ya kongamano hilo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) itafanya mkutano na wafanyabiashara Wakitanzania wenye nia ya kutafuta masoko nchini Ufaransa, tarehe 20 Aprili 2018. Ubalozi utaelezea fursa zilizopo nchini Ufaransa na mikakati ya kufanya bidhaa za Tanzania hususan za kilimo ziweze kuuzwa nchini humo.
Wizara inatoa wito kwa Wafanyabishara wa Tanzania kushiriki kikamilifu na kuchangamkia fursa hii muhimu.
No comments:
Post a Comment