Wananchi katika
Halmashauri ya mji Bariadi Mkoani Simiyu, wamejitokeza kwa wingi kujitolea
kuchangia nguvu kazi ili kuipandisha hadhi shule ya Sekondari Simiyu ili iweze
kuwa shule ya vipaji maalumu.
Aidha wameitika wito
wa Serikali ya Mkoa huo, wa kuchangia nguvukazi kwa kuanza kuchimba msingi wa
ujenzi wa vyumba vya madarasa zaidi 40 na mabweni 15 katika shule hiyo
‘’Tumekuja kujitolea nguvukazi
kujenga shule hii ambayo tayari ilikuwepo japo inaonekana kuwa na sura ya shule
za kata wakati inabeba jina la mkoa…shule hii wanasoma watoto wetu ni lazima
tuijenge na watoto wapate elimu bora kwa maisha yao ya baadae’’ Alisema
Yohana Kibusi Mkazi wa Mjini Bariadi.
Diwani wa kata ya
Malambo Kulwa Kitebo alisema Simiyu sekondari ni shule inayobeba jina la mkoa,
lakini hadhi yake ni ndogo sana ni vema wananchi wakajitolea kuijenga ili iwe
katika kiwango kizuri kimiundombinu.
Alisema yuko bega kwa
bega na wananchi kuhakikisha shule hiyo inajengwa, huku akiwataka wananchi
kuendelea kujitolea nguvukazi kukamilisha ujenzi huo.
Akishiriki ujenzi huo,
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alisema ujenzi huo ukikamilika itakuwa
ni moja ya shule bora pekee inayowakilisha mkoa, yenye vymba vya madarasa 40 na
mabweni 10.
Aliwashukuru wananchi
waliojitokeza kwa wingi kushiriki ujenzi huo ambao wamejitokeza bila
kulazimishwa ambo walikuja kushiriki ujenzi huo kwa hiari yao.
‘’Niwashukuru wananchi
waliojitokeza kushiriki ujenzi huo, hawajalazishwa na mtu, wamekuja kwa hiari
yao…Rais anataka watu wajiletee maendeleo kwa kufanya kazi, wameguswa na uamuzi
wa Serikali ya Mkoa huu, chini ya Uongozi wa Mtaka, kwamba kwa sasa Mkoa
utakuwa na shule bora itakayo kuwa inachukua wanafunzi wa vipaji maalum’’ Alisema Kiswaga.
Aliongeza shule
hiyo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 na kwamba
Mkoa wa Simiyu utakuwa katika ramani ya Mikoa yenye shule bora.
Akizungumzia ujenzi wa
shule hiyo Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka alisema Mkoa utajenga shule ya Mkoa
Mjini Bariadi (Makao Makuu ya mkoa) ambayo itatambulika kama Shule ya Sekondari
Simiyu na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 1000 huku ikiwa na miundombinu
muhimu kama maabara, vyumba vya kompyuta na mkongo wa Taifa.
Pia alisema pamoja na
kujenga Shule hiyo ya Mkoa, Serikali imedhamiria kushirikiana na wananchi
kujenga shule mbili maalumu kwa ajili ya wasichana na wavulana (Simiyu Girls na
Simiyu Boy's) ambazo zitabeba taswira ya Mkoa na kutambulisha Mkoa huo tofauti
na ilivyo sasa ambapo shule nyingi zilizopo katika Makao makuu ya Mkoa ni za
Kata.
Shule ya Simiyu
Sekondari kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 521 wa kidato cha kwanza hadi cha
nne, vyumba 10 vya madarasa vinavyotumika, vyoo matundu 6, maabara vumba
vitatu, na haina jengo la utawala.
No comments:
Post a Comment