Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia,
Wazee na Watoto imesema katika mikakati yake ya kuwatambua wagonjwa wanaoishi
na virusi vya UKIMWI pamoja na TB wameazimia kutembea maeneo yenye mikusanyiko
ya watu wengi ikiwemo baa, migodini na mahali pengine ili waweze kuwatambua
kiurahisi.
Hayo yameelezwa na serikali ya awamu ya tano kupitia
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Dkt. Faustine Ndugulile leo Aprili 23, 2018 Bungeni
jijini Dodoma kwenye kikao cha 15 mkutano wa 11 wa Bunge la 11 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, wakati akijibu la nyongeza kutoka kwa Mbunge Masoud
Abdallah aliyetaka kufahamu serikali ina mikakati gani katika kutoa elimu
maalum ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo yenye mikusanyiko ya
watu wengi zaidi.
"Serikali baada ya kuona
kumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo
wengi wamekuwa wakiathirika na ugonjwa wa TB na UKIMWI. Hivyo tumeamua
kujielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari lakini
vilevile tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi
sambamba na hilo tumetengeneza tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa
wa TB na UKIMWI", amesema
Dkt. Ndugulile.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndugulile ameendelea kwa
kusema "sasa hivi tumeanza kujielekeza mahali kwenye watu
wengi ili tuweze kuwapata kwa pamoja hususani wanaume ambapo mara nyingi
wanakuwa katika bar. Msishangae kutuona na sisi tunapita huko kuwaomba kufanya
upimaji wa suala la ugonjwa wa UKIMWI pamoja na TB".
Kwa upande mwingine, Naibu Waziri wa Afya,
Dkt. Faustine Ndugulile amesema kumgundua mgonjwa wa TB mapema na kumuweka
katika matibabu ndio njia kuu ya kupambana na kulishinda tatizo la kifua kikuu
jambo ambalo lipo kwenye mikakati ya serikali katika kufufua uwezo wa kufikia
watu wote wanaohitaji huduma za TB ili kuwagundua mapema na kuwatibu
kikamilifu.
No comments:
Post a Comment