Tuesday 3 April 2018

MKOA WA GEITA MIONGONI MWA MIKOA INAYOONGOZA KWA UTORO MASHULENI



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameitaja mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa sekondari.Waziri mkuu pia ameitaja mikoa ya Rukwa, Geita, Tabora, Singida na Simiyu kuwa inaongoza kwa utoro wa wanafunzi wa shule za msingi.

Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa ameitaja mikoa hiyo leo Jumatatu Aprili 2,2018 akizindua mbio za Mwenge wa Uhuru katika uwanja wa Magogo mkoani Geita.
Mbio za Mwenge zitakazohitimishwa Oktoba 14,2018 mkoani Tanga zinaongozwa na kauli mbiu “Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya nchi yetu.”

Majaliwa amesema Mkoa wa Tabora unaongoza kwa asilimia 9.7 ya wanafunzi watoro wa sekondari ukifuatiwa na Geita (asilimia 8.1), Mtwara (asilimia 6.1) na Shinyanga (asilimia 6.3).
Kwa shule za msingi, Rukwa inaongoza kwa asilimia 3.2, ukifuata Geita (asilimia 3.1), Tabora (asilimia 2.9), Singida (asilimia 2) na Simiyu (asilimia 2).

“Kwa jumla utoro wa wanafunzi wa sekondari ni mkubwa kuliko shule za msingi. Naikumbusha mikoa yote niliyoitaja kuhamasisha wananchi wakiwamo wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni kwa kutumia utaratibu wa sheria zilizowekwa,” amesema Majaliwa.

Aidha , Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mheshimiwa Jensita Mhagama ameelezea kuwa mwenge ni Chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa ,Mwl Julius Kambarage Nyerere Mwaka 1961 ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika.

“Mbio za mwenge wa uhuru zilianza rasimi mwaka 1964 baada ya mapinduzi matukufu ya Zanzibar uliozaa nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”Alisema Waziri Jenista.

Mwenge wa uhuru utakimbizwa katika  mikoa yote 31 ya Tanzania  katika halmashauri 195 na  kwa muda wa siku 195.

Sherehe hizo zilizosindikizwa na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili, kwaya, na halaiki zilifana huku zilihuidhuriwa na wakazi wengi.

Huku kauli mbiu ikiwa ni” Elimu ni ufunguo wa maisha ,wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa”

No comments:

Post a Comment