Mkuu wa wilaya ya Geita Mwalimu Herman Kapufi amekutana na watendaji wa mitaa,vijiji, kata,elimu na afya kutoka Halmashauri za wilaya na Mji Geita kuwapa maagizo ya kukabiliana na tatizo la utoro sugu na rejareja kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani hapa.
Aidha amewataka watendaji hao kutoa taarifa sahihi na haraka kwa uongozi wa wilaya kwa familia zote ambazo watoto wametoroka shule na kwenda kufanya shughuli mbalimbali za majumbani, migodini, uvuvi na wale ambao wameozeshwa na familia zao.
Pia hakusita kuwaonya watendaji ambao wamekua wakipokea kesi za wanafunzi kupewa mimba na baadhi ya watu maarufu vijijini kutofikisha taarifa kwa uongozi wa wilaya na pia kawakemea viongozi wa kisiasa ambao huwasaidia watuhumiwa wa utoro na mimba kutochukuliwa hatua.
“Msibague mtu katika ukamataji huo, kumekua na tabia ya wanyonge kuonewa katika matukio mbalimbali nawaomba hata wenye nguvu kama wametenda makosa wakamatwe na wafikishwe mahakamani.”alisema DC Kapufi.
Vikao hivi ni moja ya mkakati wa Mkuu wa wilaya ya Geita kuwapa maagizo watendaji wote wa serikali kuhakikisha wanaondoa tatizo la utoro na mimba mashuleni kwani Wilaya ya Geita inashika nafasi ya pili kulinganisha na wilaya zingine Mkoani hapa..
No comments:
Post a Comment