Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za
Mitaa (TALGWU) kimefunguka na kumwagia sifa Mbunge wa jimbo la Geita Mjini,
Joseph Kasheku maarufu kama Musukuma kwa kulivalia njuga suala la watumishi wa
umma waliofukuzwa kazi wenye sifa ya darasa la saba, na mpaka serikali kuamua
kuwarudisha kazini.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Rashid
Mohamed Mtima wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari leo
baada ya kupita siku moja tokea serikali ilivyotoa kauli yake kupitia Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika ya kuagiza
watumishi wa umma 1,370 walioajiriwa kabla ya Mei 20, 2004 ambao hawakufaulu
mtihani wa kidato cha nne, (darasa la saba) na waliondolewa kazini kwa kigezo
cha vyeti vya kidato cha nne, warudishwe kazini mara moja na wapewe stahiki zao
zote ikiwemo mishahara yao tangu walipoachishwa kazi.
"Suala hili sisi tumeanza muda
mrefu kulihangaikia lakini'last week' tuliwaona wabunge walivyokuwa
wamechachamaa Bungeni wakiwa ongozwa na Mbunge wa jimbo la Geita Mjini, Joseph
Kasheku Msukuma kwa kuweza kulipigia kelele jambo hili tunawashukuru sana, kwa
maana hata kama lingekuwa lipo kwenye mchakato la kufanyiwa kazi lakini wao
waliliongezea kazi zaidi mpaka serikali ikatangaza kuwarudisha kazini", amesema Mtima.
Pamoja na hayo, Mtima ameendelea kwa
kusema "kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za
Mitaa (TALGWU), napenda kutoa shukrani kwa serikali ya awamu ya tano kwa
kuzingatia mapendekezo tuliyowasilisha serikalini Machi 22, 2018 na hatimaye
jana yakafanyiwa kazi. Kwa kweli jambo hili tunashukuru sana kwa maana serikali
imekuwa sikivu. Pia tunapenda kutoa shukrani kwa Waziri Mkuu kwa namna
alivyoweza kutusaidia kipindi tulivyokuwa tunahangaikia mchakato huu".
Kwa upande mwingine, Mtima amesema wanachama
wake wamefurahishwa na uamuzi huo wa serikali kwa kuwa umeweza kurudisha
matumaini mapya kwa watumishi hao waliofukuzwa kazi hapo awali.
No comments:
Post a Comment