Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
Kushoto akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Wanane wa Taasisi za Uwekezaji kutoka
Nchini Misri hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Kiongozi wa Ujumbe wa Viongozi Wanane wa Taasisi za Uwekezaji
kutoka Nchini Misri Bwana Amgad Hassoun wa Pili kutoka Kulia akimueleza Balozi
Seif maeneo ambayo Kampuni za Misri zinaweza kuwekeza Miradi yao Visiwani
Zanzibar. Picha na – OMPR – ZNZ.
Zanzibar inaweza
kuimarika zaidi kiuchumi, Maendeleo na Ustawi wa Jamii endapo uwekezaji katika
Sekta ya Utalii, ujenzi wa Miji Mipya ya Nyumba za Makaazi ya Wananchi wa
kawaida, Uvuvi, pamoja na Mifugo itajengewa miundombinu imara katika utekelezaji
wake.
Hayo yamejiri kufuatia
Kikao cha pamoja kati ya Ujumbe wa Wawekezaji Wanane kutoka Nchini Misri
ukiongozwa na Bwana Amgad Hassoun ulipozungumza na Ujumbe wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ukiongoza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.
Mmoja wa Viongozi wa
Ujumbe huo kutoka Misri Profesa Hossam El – Borombaly alisema zipo Taasisi na
Makampuni ya Uwekezaji Nchini Misri yenye uwezo wa kuwekeza katika Sekta za
Uvuvi, Miji Mipya, Mifugo na Miradi ya Utalii lakini kinachohitajika ni namna
ya kuitekeleza kupitia Mikopo ya Benki zilizojitolea kusimamia Miradi hiyo.
Profesa Hossam alisema
ujenzi wa Miji ya Kisasa ambayo Misri imeshakuwa na uzoefu mkubwa inaweza
kustawisha Wananchi wa Kipato cha chini kwa kupata Makaazi bora sambamba na
upatikanaji wa Ofisi zenye hadhi inayokubalika Kimataifa.
Alieleza kwamba mradi
huo unazingatia hali halisi ya Kimazingira hasa ikitiliwa maanani mfumo wa
misimu ya hali ya hewa kama ule wa masika wakati mwengine huambatana na mvua
kubwa zinazosababisha mafuriko na kuleta Maafa.
Alisema Sekta ya Uvuvi
kwa upande wake inaweza kutoa ajira kubwa kwa vile Zanzibar imebarikiwa
kuzunguukwa na Bahari pande zote baraka ambayo uwezo wa kuvuliwa Tani 1,000 za
samaki unawezekana kabisa.
Naye kiongozi wa Ujumbe
huo Bwana Amgad Hassoun alisema upo uwezekano mkubwa wa Kamapuni ya Taasisi za
kusafirisha Watalii za Misri kuwa kiunganishi cha safari za Watalii kutoka Nchi
za Bara la Asia ambao wameonyesha nia ya kutaka kutembelea Visiwa vya Zanzibar.
Bwana Amgad alisema
utafiti umebaini kwamba Watalii wengi kutoka Nchi za Kazakistan, Ubakistan
pamoja na Pakistan wameonyesha shauku na tayari wanapenda kuitembelea Zanzibar
baada ya kupata sifa ya ukarimu wa Watu wake unaozingatia Mila na Utamaduni
wake.
Kwa upande wake Waziri
wa Kilimo, Mali Asili, Mifugo na Uvuvi Mh. Rashid Ali Juma ambae aliwahi kuwa
Waziri anayesimamia Sekta ya Utalii aliueleza Ujumbe wa Wawekezaji hao kutoka
Nchini Misri kwamba, Wawekezaji wenye nia ya kutaka kuanzisha Miradi yao
Zanzibar wanapaswa kuzingatia Utamaduni na Mila za Watu wake.
Mh. Rashid alisema hatua
hiyo inasaidia na kuharakisha kukamilisha kwa haraka malengo ya Wawekezaji hao
yanayokwenda sambamba na utayari wa Wananchi wa maeneo yatakayohusika na Miradi
hiyo ya uwekezaji.
Akitoa shukrani zake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe huo wa
Misri kwamba Zanzibar bado ina maeneo mengi ya uwekezaji yanayopaswa
kuchangamkiwa na Makampuni na Taasisi za Uwekezaji kutoka Nchini Misri.
Balozi Seif aliwaomba
Viongozi wa Ujumbe huo kuangalia maeneo ambayo wanaweza kujitokeza kuwekeza na
kuwataka kuainisha Miradi watakayoilenga kuanzisha katika maombi watakayotuma.
Othman
Khamis Ame
Ofisi
ya Makamu ya Pili wa Rais wa Zanzibar
16/4/2018.
No comments:
Post a Comment