Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba
Makubaliano ya Paris
chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi
utainufaisha nchi kwa kuimarika kwa Mipango ya Taifa ya kuhimili athari za
mabadiliko ya tabianchi ili kupunguza majanga yatokanayo na athari hizo.
Hayo yameelezwa leo
Bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira Mhe. January Makamba wakati akiwasilisha Azimio la Bunge la kuridhia
makubaliano ya mkataba huo.
"Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa kuweka saini makubaliano hayo na hatimaye kuyatekeleza
itanufaika na mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha hali ya uchumi wa nchi na
kujenga uchumi endelevu wa viwanda wenye kustahimili mabadiliko ya
tabianchi," alisema Mhe. Makamba.
Makamba
Amesema, Mkataba huo utaongeza upatikanaji wa fursa zilizopo za
miradi na teknolojia safi itakayowezesha matumizi ya gesi asilia majumbani na
viwandani ili kuchochea maendeleo ya viwanda kwa kutumia nishati yenye bei
nafuu.
Vilevile, utaimarisha
ushirikiano baina ya Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa katika kusimamia na
kutekeleza masuala yanayohusu mabadiliko ya tabianchi.
"Makubaliano ya
Paris yanalenga kuboresha utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa
mwaka 1992 kwa kutunza misitu inayonyonya joto, kuandaa na
kutekeleza mipango ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kuwa na mifumo ya
upatikanaji wa fedha na teknolojia safi kwa nchi zinazoendelea ili kukabiliana
na changamoto ya tabianchi," alifafanua Mhe. Makamba.
Aidha amesema, kwa
kuzingatia manufaa yatokanayo na Mkataba huo pamoja na itifaki yake kwa
Tanzania na pia umuhimu na manufaa ya makubaliano hayo, Bunge katika Mkutano
wake wa Kumi na Moja na kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3)(e) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, linaazimia kuridhia makubaliano ya Paris
kuhusu kuboresha utekelezaji wa Mkataba wa mabadiliko ya Tabianchi yaani "THE
PARIS AGREEMENT UNDER THE UN FRAMEWORK CONVENTIN ON CLIMATE CHANGE".
No comments:
Post a Comment