Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imesema hadi kufikia Juni 30 mwaka huu
inatarajia kuajiri walimu 6,000 wa masomo ya Hisabati na Sayansi kwa ajili ya
shule za sekondari nchini.
Kauli hiyo ilitolewa
jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda,
alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali,
ambaye alitaka kujua mikakati ya serikali katika kuondoa changamoto katika
shule za kata ikiwamo upunguzu wa walimu wa Hisabati na Sayansi.
Pia, Bobali alitaka
kujua msimamo wa serikali kuhusu wananchi kuchangia kwenye chakula ambacho
wameona ndio chachu ya kuongeza ufaulu kwa wanafunzi katika Mkoa wa Lindi.
Alisema hadi Desemba mwaka 2017, Serikali ilikuwa imeajiri walimu 200 wa
Hisabati na Sayansi kwa ajili ya shule za sekondari.
Kadhalika, alisema
serikali haijazuia wananchi kuchangia maendeleo ya shule walichokataza ni
kumzuia kumpa adha ya kukosa masomo mwanafunzi ambaye ameshindwa kuchangia
michango hiyo.
Katika swali la msingi,
Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali imefanya tathmini juu ya ubora na
changamoto zilizopo katika shule za sekondari za kata nchini.
Akijibu Kakunda alisema
hadi Oktoba 2017, Shule za kata 3,103 zilikuwa na wanafunzi 197,663 ambao kama
zisinge kuwepo wangeikosa elimu ya sekondari.
Kakunda alisema maamuzi
ya kuanzishwa kwa shule ya sekondari kila kata ili kuhakikisha watoto wengi
zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo ya sekondari licha ya kufaulu
mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu ya uchache wa shule wanapata nafasi
hizo.
Alisema tathmini mbili
za serikali zilizochambua kwa kina sekta ya Elimu kupitia Tume ya Prof. Mchome
ya mwaka 2013, iliyochambua sababu za ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye
mitihani ya mwaka 2012 na kamati ya kuhuisha na kuoanisha sera ya Elimu na
Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya mwaka 1996.
Pia alisema sera ya
Taifa ya Elimu ya juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano kwa elimu ya msingi ya mwaka 2007, iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar
Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na kuishauri serikali kuanzisha sera mpya
moja ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.
No comments:
Post a Comment