Kaya
6120 sawa na asilimia 52 ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi
Mkoani Simiyu zimewezeshwa kulima pamba ekari 8712 katika Msimu wa mwaka
2017/2018 kwa kutumia fedha za uhawilishaji.
Hayo
yalibainishwa na Mratibu wa TASAF Mkoa wa Simiyu Bw. Nyasilu Ndulu
wakati wa kikao cha kujenga uelewa wa pamoja kwa viongozi
juu ya mpango huo kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT mjini Bariadi.
Nyasilu
amesema pamoja na kulima pamba walengwa wa mpango huo katika Wilaya ya Bariadi
na wilaya nyingine Mkoani Simiyu, kupitia fedha za uhawilishaji (wanazopewa)
wamefanikiwa kujenga nyumba, kufuga, kuanzisha biashara ndogo ndogo na kujiunga
na Mfuko wa Afya ya Jamii(CHF).
Ameongeza
kuwa tangu kuanza kwa zoezi la uhawilishaji chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini awamu ya tatu mwaka 2015 hadi sasa, tayari awamu
17 za malipo zimekwisha fanyika kwa walengwa 37, 533 na jumla ya
shilingi bilioni 28.9 zimelipwa kwa wahusika.
Amesema fedha
hizo zimejumuisha ruzuku za aina mbili ikiwa ni ruzuku ya msingi na ile
itokanayo na utimizaji wa mashati ya Afya na Elimu ambapo watoto 39,068 sawa na
asilimia 90.3 wameweza kupata mahitaji muhimu ya shule na kukuhudhuria shuleni
na watoto 51, 280 sawa na asilimia 93.1 wamepata mahitaji ya kliniki na
kupelekwa kliniki.
“Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini umeweza kuwasaidia
walengwa kujikwamua kutoka kwenye umaskini, wapo walioanzisha biashara,
wanaolima, wanaofuga, waliojenga nyumba bora; kwa kutumia fedha hizi wanazopewa
wapo ambao watoto walikuwa hawahudhurii shuleni na kliniki lakini sasa hivi
mahudhurio mazuri” Alisema.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka awali akifungua kikao amesema pamoja na
mafanikio waliyoyapata walengwa, wanufaika wote waliofanya mambo ya
maendeleo ni vema wakawa mfano kwa wenzao huku akiwataka wale walioshindwa
kuondolewa kwenye mpango huo.
Aidha,
Mtaka aliwataka walengwa wote wa mpango kuendana na
malengo ya nchi ya kuelekea kwenye Uchumi wa Kati ifikapo mwaka 2025 badala ya
kuwaza kuendelea kubaki katika mpango huo.
“Mtazamo
wangu mimi ni vizuri wanufaika wa TASAF waendane na Mpango wa Nchi, tunaposema
tunataka kwenda kwenye Uchumi wa Kati kufikia mwaka 2025 wanufaika wa TASAF
wanapaswa kujindaa kwenda kwenye uchumi wa kati, ili badala ya watu kutaka tu
kuingia kwenye mpango, tupate watu wanaotaka kutoka baada ya kupiga
hatua na kutoka kwenye umaskini waliokuwa nao mwanzo” alifafanua Mtaka
Nae
Bw. Fariji Mishael mtaalamu wa ufuatiliaji wa tathmini kutoka Ofisi ya TASAF
Makao makuu aliupongeza Mkoa wa Simiyu kwa kutekeleza mpango huo vizuri
na kuomba wataalamu kuwasaidia walengwa walio kwenye maeneo yao katika
kuwashauri namna bora ya kuendesha miradi waliyoianzisha ili iwe endelevu na
iweze kuwasaidia kiuchumi.
No comments:
Post a Comment