Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira na Muungano, Mhe. January Makamba
Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inaendelea kufanya juhudi mbalimbali ili
kuhakikisha changamoto zilizopo katika Muungano kati ya Serikali ya Tanzania na
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zinatatuliwa.
Utatuzi
huu unafanyika kwa njia ya vikao vya pamoja baina ya Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na ile ya Mapinduzi Zanzibar.
Hadi
kufikia mwaka 2017, jumla ya changamoto 12 kati ya 15 zilizokuwepo mwaka 2006
tayari zilishapatiwa ufumbuzi wakati 3 zilizobakia zinaendelea kutafutiwa
ufumbuzi wake.
Changamoto
3 zinazoendelea kutafutiwa ufumbuzi ni Tume ya pamoja ya Fedha inayohusu makato
na gharama za kuchangia shughuli za Muungano, Hisa za Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki pamoja na Usajili wa Vyombo
vya Moto.
Katika
kikao cha kamati ya pamoja ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar cha Aprili, 2017 kilichojadili
kuhusu changamoto za Muungano, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais
anayeshughulikia Mazingira na Muungano, Mhe. January Makamba alisema kuwa
baadhi ya masuala yenye changamoto yanahitaji utaratibu wa kubadilishwa kwa
baadhi ya Sheria kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na baadaye
yaridhiwe na Baraza la Wawakilishi.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umeleta
maendeleo na mafanikio makubwa katika kuijengea nchi heshima, umesababisha
kuwepo kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongezeka kwa usalama wa
nchi pamoja na kuongezeka kwa ushirikiano katika masuala yasiyo ya kimuungano.
Aidha,
ili kuimarisha Muungano huo kwa pande zote mbili utaratibu umeshaandaliwa wa
Viongozi Wakuu wa Upande wa Tanzania Bara wa kufanya ziara za kukagua miradi ya
maendeleo kwa upande wa Zanzibar.
Pia,
ili kufaidika na ujio wa viongozi wa kimataifa, Waziri Mkuu wa Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliiagiza Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuandaa utaratibu mzuri ili
wakati wa ujio wa Viongozi Wakuu wa Mataifa ya Nje wanaofanya ziara Tanzania
Bara pia wafike Zanzibar.
Aliyekuwa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira, Mhe. Samia
Suluhu Hassan wakati alipotembelewa na Balozi wa Uingereza nchini Diana Melrose
mnamo mwaka 2013 alisema, ni bora kuendelea na Muungano kuliko kuuvunja na
kushauri kuwa mabadiliko yafanyike ili kuuboresha.
Kuungana
kwa Tanganyika na Zanzibar sio jambo la kushangaza kwani kuna nchi nyingi
duniani zilishaungana zikiwemo za Siria na Misri walioungana mwaka 1958 pamoja
na muungano wa Yemen ya Kaskazini na Yemen ya Kusini walioungana mwaka 1990.
Kati
ya nchi zilizoungana, nyingi zimeshindwa kuendeleza muungano baina yao kwa
sababu ya kukosa mifumo thabiti ya kushughulikia masuala hayo kwa kutolea
mfano muungano
wa Siria na Misri ambao ulidumu kwa miaka 3 na kuvunjika mwaka 1961.
Hivyo,
ili kuendeleza ushirikiano na umoja uliopo baina ya Tanganyika na Zanzibar,
wananchi tuache kutumia changamoto zilizopo katika Muungano huu ambazo
zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kwa njia ya majadiliano yanayohusisha pande
zote mbili kama silaha ya kuharibu Muungano.
Vile
vile tuache kuchanganya Muungano wetu na masuala mengine kwani mbali na
changamoto zilizotajwa, dini na siasa imeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa
kutaka kuharibu Muungano huu wenye manufaa mengi kwa pande zote mbili.
Tunapoelekea
kuadhimisha miaka 54 ya kuwepo kwa Muungano huu kila mwananchi ajitafakari
namna ambavyo atashiriki katika kukuza maendeleo ya kiuchumi ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania hasa katika ujenzi wa viwanda unaotiliwa mkazo na Serikali
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Muungano
huu umedumu na utaendelea kudumu na kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.
No comments:
Post a Comment