Thursday, 19 April 2018

HUDUMA ZA MAJI ZAIMARIKA, TEKNOLOJIA KUONDOA MATUMIZI YA MKAA


Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe akijibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  katika Wizara yake mapema mjini Dodoma  wakati wa mkutano na waandishi wa habari ( hawapo pichani).


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January   Makamba akijibu hoja mbalimnbali zilizobainishwa katika ripoti  ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  katika Ofisi hiyo mapema mjini Dodoma wakati wa mkutano na waandishi wa habari (hawapo pichani).


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akisisitiza kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utaratibu wa Mawaziri wote kukutana na waandishi wa habari kujibu hoja mbalimbali zilizobainishwa katika  ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)  katika Wizara zao mapema mjini Dodoma.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi akifurahia jambo na Naibu Waziri wa Maji Mhe. Jumaa  Aweso  mapema mjini Dodoma wakati wa mkutano  na waandishi wa habari uliowashirikisha  Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January  Makamba. (Picha zote  na Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma)

Upatikanaji wa maji mijini na vijijini umeimarika kutoka chini ya 50% ya awali kutokana na umakini katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji safi nchini. Aidha, ili kukabiliana na mazingira Serikali imeanza mchakato wa kutumia mifumo ya kisayansi ili kuondoa matumizi ya mkaa majumbani.

Hatua hizo zimebainishwa na Mhe. Isack Kamwelwe, Waziri wa Maji na Umwagiliaji na Mhe. Januari Makamba, Waziri wa Nchi (Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira) walipokuwa wakieleza utekelezaji wa hoja za CAG katika sekta zao.

Akizungumzia hoja kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji nchini, Waziri Kamwelwe amesisitiza kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, ufuatiliaji na kuzibwa mianya ya ubadhirifu vimeleta mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini.

“Sisi kwa upande wetu CAG anatuonesha njia ili tufanye vizuri zaidi. Hadi kufikia Desemba, 2017, upatikanaji wa maji mijini umepanda hadi kufikia asilimia 78. Kwa upande wa vijijini, hadi kufikia Machi 2018, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imejenga vituo vya kuchotea maji 123,888 vyenye uwezo wa kuhudumia takribani watu milioni 30 sawa na asilimia 68.8,” Alisema.

Kwa upande wake, Waziri Makamba amesema hoja za CAG zimewasaidia kuongeza mikakati hasa ya kutumia sayansi na teknolojia kupata mbadala wa matumizi ya mkaa ili kuokoa misitu na kutunza mazingira. Amesema tayari Ofisi yake na wadau wanafanya majaribio ya baadhi ya teknolojia hizo.

Kuhusu changamoto za kupambana na taka za kielektroniki, amekiri kuwa Tanzania kama nchi nyingine zinazoendelea inakumbana na changamoto ya kupokea vifaa vingi vilivyotumika kama kompyuta, simu na chaja ambavyo huharabika haraka na kutupwa kama taka za kielectroniki.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeanza kutoa vibali kwa makampuni 16 yenye utaalamu kwa ajili ya kukusanya, kusafirisha na kurejeresha (recycling) taka za kielektroniki,” Alisema.

Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.

No comments:

Post a Comment