Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji
Serikali imeahidi
kuboresha miundombinu na fursa nyingi za kiuchumi katika maeneo ya vijijini ili
kuweka mazingira bora na salama yatakayovutia wawekezaji katika sekta
mbalimbali hususani Sekta ya Fedha.
Hayo yameelezwa Bungeni
mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb)
alipokuwa akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kalenga (CCM) Mhe. Godfrey
Mgimwa aliyetaka kujua tamko la Serikali juu ya idadi kubwa ya benki za
biashara kufunguliwa kwenye miji mikubwa.
Akijibu swali hilo Dkt.
Kijaji alisema kuwa miji mikubwa inakidhi vigezo muhimu vya uwekezaji kwa Sekta
ya Fedha kama vile uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi, miundombinu ya kisasa na
usalama ikilinganishwa na maeneo ya vijijini.
Alisema kuwa kufuatia
mabadiliko ya mfumo wa kiuchumi nchini unaotekelezwa tangu mwanzoni mwa miaka
ya 1990, shughuli nyingi za kiuchumi hususani benki zinaendeshwa na Sekta
Binafsi .
“Kwakuwa Sekta Binafsi
lengo lake ni kufanya biashara na kupata faida, uwanzishaji wa huduma za
kibenki hutegemea upembuzi yakinifu ambao unazingatia fursa za kiuchumi
zilizopo katika eneo husika, uwepo wa miundombinu wezeshi na usalama”, alisema
Dkt. Kijaji.
Alifafanua kuwa Serikali
inachokifanya ni kuweka mazingira bora yatakayowavutia wawekezaji wa ndani na
nje kuwekeza maeneo ya vijijini kwa kuwa lengo ni kufikisha huduma za kifedha
kwa watanzania wote.
Katika swali la nyongeza
la Mbunge huyo, alitaka kujua mbinu mbadala ya Serikali kuhakikisha inapeleka
huduma za benki vijijini, kwa kuwa mpaka sasa Serikali bado haijaunda Sera ya
kuhakikisha huduma hizo zinawafikia walengwa hasa wa vijijini.
Dkt. Kijaji alieleza
kuwa mpango mbadala wa kuhakikisha huduma za kibenki zinafika vijijini upo na
Serikali inausimamia vizuri, na kuongeza kuwa mpango huo umeiwezesha Tanzania
kuongoza katika huduma za fedha jumuishi barani Afrika.
Aidha Dkt. Kijaji
alifafanua kuwa uwepo wa mawakala wa benki, kutolewa kwa huduma za kibenki
kupitia Kampuni za simu ni ishara tosha kuwa Serikali imekuwa ikijitahidi
kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote.
No comments:
Post a Comment