Mkuu wa wilaya ya Geita Mheshimiwa Herman Clement Kapufi amewashauri
wananchi wa Wilaya ya Geita kuwekeza nguvu zao katika kilimo cha mazao ya
Kahawa na miwa ya sukari ambayo yameonekana yanastawi vizuri katika ukanda wa
ziwa viktoria
Mwl. Kapufi ametoa ushauri huo wakati alipofanya ziara ya kikazi kwa
kuwatembelea wakulima wa mazao hayo ambao wameamua kuingia katika kilimo hicho
kufuatia ushauri waliopata kutoka kwa wataalamu wa kilimo kutoka Halmashauri
kwa kushirikiana na bodi ya sukari Tanzania pamoja na wataalamu kutoka Maruku
mkoani Kagera.
Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia idara ya Kilimo na Umwagiliaji
imeamua kuanzisha kilimo cha mazao ya Kahawa na Miwa ambayo hayakupewa
kipaumbele hapo awali kwenye wilaya hiyo.
Kufikia msimu wa kilimo wa 2014/2015 jumla ya miche ya mibuni 41,808 ya
kutosheleza hekta 8.6 ambazo ni sawa na ekari 33.2 kati ya lengo la hekta 49
zilisambazwa na kupandwa katika mashamba ya wakulima kwa kata za
Nzera,Lwezera,Kakubilo,Nkome,Nyamboge,Senga,Nyamwilolelwa,Chigunga,Bukondo na
Nyakagomba ambazo zina hali nzuri ya hewa inayostahimili kustawi vyema kwa
kilimo cha kahawa.
Upande wa kilimo cha miwa kilianzishwa mwaka 2015 na jumla ya ekari
75.5 zimelimwa katika maeneo ya Nzera, Lwezera, Chigunga na Nyamwilololwa kwa
ufadhili wa bodi ya sukari Tanzania.
Miwa hiyo hukomaa baada ya miezi minane 8 na uzalishaji wake kwa ekari
moja ni tani 40 kama imetunzwa vyema na baada ya uzalishwaji inatarajiwa kuuzwa
kwa bei ya shilingi 60,000/= kwa tani.
Akiongea na waandishi wa habari na wataalamu ambao alifuatana nao katika
ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Geita Mh Herman Clement Kapufi amesema yuko tayari
kuwasaidia wakulima wa Kahawa ambao atahakikisha wanapata mafunzo bora ya
kilimo hicho na linakua ni zao mmbadala la biashara kwa wakulima wa Geita
badala ya kutegemea dhahabu pekee na kwamba wajue pia hata kilimo ni
utajiri.
Kwa Upande wa afisa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Geita
anayeshughulikia mazao ya biashara ndugu Samwel Abuya amesema kwa msimu wa kilimo
wa wa mwaka 2015/2016 jumla ya tani 5.5 sawa na kilo 5,500 zenye thamani ya
shilingi za Kitanzania 8,800,000/= zilizalishwa na wakulima wa zao hilo kwa
Halmashauri ya wilaya ya Geita pia kuna wakulima wengine 530 ambao wamehamasika
kupanda zao la kahawa na tayari wamejiandikisha kupata miche hiyo ili waweze
kujiunga kwenye zao hilo la biashara.
No comments:
Post a Comment