Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha wananchi(CUF)hicho Saverina Mwijage.
Chama cha wananchi (CUF) Bukoba kimejiandaa kufanya maandamano ya amani
keshokutwa, kwa ajili ya kupinga kufanyika upya uchaguzi wa Zanzibar
unaotarajiwa kuwa Machi 20 mwaka huu.
Kimeiomba pia serikali ya awamu ya tano, kuchukua uamuzi wa
kumtambua Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa urais
Zanzibar na kuwa hakiko tayari kurudia uchaguzi huo tena.
Akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wa chama
hicho, Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho Saverina Mwijage, alisisitiza kuwa kamwe
chama hicho hakitakuwa tayari kurudia uchaguzi huo uliotangazwa na Tume ya
uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa utafanyika Machi 20,kwa kile kinachodaiwa ni kufutwa
uchaguzi wa Oktoba 25,mwaka jana.
“Tumedhamiria
kuandamana ili kumfikishia ujumbe wetu Rais John Magufuli kupitia kwa Mkuu wa
mkoa wa Kagera, John Mongella lengo letu hasa ni kupinga uchaguzi wa Zanzibar.
Hali ya Zanzibar kwa sasa haiko shwari, watu wanatishiwa maisha yao, wanaishi
kwa hofu juu ya maisha,” alisisitiza.
Mwijage ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake
wa CUF Taifa, alisema chama hicho kinatambua uchaguzi ulishakwisha na tume hiyo
ilishatoa vyeti kwa walioshinda, kwa mantiki hiyo CUF inamtambua Maalim Seif
kuwa alishinda katika uchaguzi huo.
Alisema maandamano hayo yanatarajiwa kuanzia saa 4:00 asubuhi
hadi saa 9:00 alasiri na baadaye utakuwepo mkutano wa hadhara katika Uwanja wa
Mashujaa Mayunga ulioko mjini Bukoba ili kuutangazia umma juu ya msimamo wa
chama hicho na baada ya hapo watazunguka katika wilaya za Muleba, Missenyi na
Karagwe.
No comments:
Post a Comment