Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel akisisitiza umuhimu wa kuheshimu wanawake wakati akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yanayoadhimishwa kimkoa katika Wilaya ya Bukombe Mkoani humo.
Baadhi ya wanawake Wilayani Bukombe wakifatilia maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yanayoadhimishwa kimkoa katika Wilaya hiyo Mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel akiongoza zoezi la ukataji keki kabla ya kuhutubia wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yanayoadhimishwa kimkoa katika Wilaya ya Bukombe Mkoni humo.
Mbnge wa Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu Waziri wa madini Mhe Doto Mashaka Biteko akichangia shilingi 500,000 kuunga mkono harambee iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel ambaye naye alichangia shilingi laki tano kwa ajili ya jukwaa la wanawake Jimbo la Bukombe
Wakurugenzi wa Halamshauri za Wilaya katika Mkoa wa Geita wamekumbushwa
kutekeleza wajibu wao kwa kutenga fedha asilimia 4 kwa ajili ya mfuko wa
maendeleo ya wanawake, asilimia 4 kwa ajili ya mfuko wa maendeleo ya vijana na
asilimia 2 kwa ajili ya watu kwenye ulemavu.
Wakurugenzi hao wametakiwa kuongeza kasi katika kuendelea kuchambua na
kutambua vikundi vya wanawake na vijana vyenye mwelekeo wa kuzalisha Mali ghafi
kwa ajili ya kulisha viwanda vidogo na vya kati ili kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendeleo.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert Gabriel wakati
akihutubia wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake
Duniani yaliyoadhimishwa kimkoa katika Wilaya ya Bukombe.
Alisisitiza kuwa vikundi hivyo vinapaswa kujengewa uwezo wa kifedha,
mafunzo pamoja na vifaa na hatimaye viweze kuchangia katika azma ya Serikali ya
Tanzania ya uchumi wa viwanda kwani kupitia fursa hizo wanawake wengi
watajiajiri na kuajiri watu wengine katika sekta isiyo rasmi.
Alisema kuwa sambamba na kuwajengea uwezo wanawake lipo jukumu la
kuwalinda wanawake hao pamoja na wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili kimwili
kama vipigo, ubakwaji, ndoa za utotoni na kuwarubuni kimapanzi wabinti wadogo.
Aidha, amezitaka mamlaka zote ndani ya Mkoa wa Geita kuhakikisha zinatoa
ushirikiano kwa wajumbe wa kamati zinazoundwa katika ngazi zote ili kwa pamoja
kuhakikisha vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto
vinatokomezwa.
Katika hatua nyingine Mhe Gabriel amezitaka Halmashauri za Wilaya
kushirikiana na wadau mbalimbali kutenga bajeti na kuendelea kuweka mipango
shirikishi ya kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili wanawake na wasichana
ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu na usalama wa
mtoto wa kike na kulinda mustakabali wake kwa kumuwezesha kiuchumi, kielimu,
kiafya na kumlinda dhidi ya vitendo vya ukatili kimwili.
Alisema kuwa kauli mbiu ya Kitaifa kwa mwaka huu ni "KUELEKEA
UCHUMI WA VIWANDA: TUIMARISHE USAWA WA KIJINSIA NA UWEZESHAJI WANAWAKE
VIJIJINI" imeakisi dira ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa muktadha wa kuhakikisha Tanzania inakuwa ni
nchi ya uchumi wa viwanda.
Alisema Serikali inatambua nguvu na ufanisi wa wanawake kwani kupitia
vikundi vya kiuchumi, VICOBA, SACCOS na vikundi vya kijamii wamekuwa
wakijihusisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi; Uchakataji wa malighafi ili
kuongeza thamani, biashara ndogondogo, ufugaji ushonaji nguo, kilimo cha mazao,
bustani za mbogamboga na matunda na nyinginezo.
Katika maadhimisho hayo Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mhe Doto Mashaka
Biteko amewapongeza wanawake Duniani kote kwa maadhimisho hayo ya siku muhimu
kwao huku akiahidi kuongeza ushirikiano kupitia vikundi vya mbalimbali ambavyo
ni msingi wa ustawi na uimara wa Jumbo hilo na Taifa kwa ujumla wake.
Sambamba na hayo pia Mhe Biteko amechangia shilingi laki tano (500,000)
kwa kuunga mkono harambee iliyoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe Robert
Gabriel ambaye naye alichangia shilingi laki tano kwa ajili ya jukwaa la
wanawake Jimbo la Bukombe.
No comments:
Post a Comment