Serikali imesema kuwa
hakuna chombo chochote cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kuandika habari
zenye mrengo wa kukosa sera na utekelezaji wake kama ambavyo wadau wengi
wamekuwa wakiaminisha umma.
Kauli hiyo imetolewa
leo na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Dkt. Hassan Abbasi wakati
akizungumza katika Kipindi cha Habari Kuu kinachorushwa na Kituo cha Televisheni
cha Startv mjini Dodoma.
Dkt. Abbasi amesema
kuwa Sheria namba 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51 kinatoa
ruhusa kwa chombo cha habari kukosoa kwa lengo la kuonyesha njia mbadala katika
kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
“Hakuna chombo cha
habari kitakachochukuliwa hatua kwa kukosoa, haki hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria
ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51, tutaendelea kuthamini na
kufanyia kazi ukosoaji huo,” alisema Dkt. Abbasi.
Hata hivyo Dkt. Abbasi
amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kwa chombo kitakachokiuka
sheria na misingi ya maadili ya taaluma ya habari kwa lengo la kulinda maslahi
ya taifa.
Dkt. Amesisitiza kuwa
ni vyema wamiliki wa vyombo vya habari wakatumia uhuru huo wa kisheria kuchapisha
habari zenye nia njema kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi badala ya kueneza
hofu miongoni ya mwa jamii.
Akijibu swali la
muongozaji wa Kipindi kuhusu kufungiwa kwa Gazeti la Mawio, Dkt. Abbasi amesema
kuwa Gazeti hilo halijafungiwa kutokana na kuandika habari ya kukosoa Serikali
isipokuwa limekiuka miiko ya taaluma kwa kuandika habari za kushushia heshima
na hadhi ya mtu katika jamii pamoja na kukiuka maagizo halali ya Serikali.
Alisema kuwa kama
ingekuwa kulifungia Gazeti hilo kwa sababu ya kuandika habari za kukosoa
pengine lingekuwa limefungiwa muda mrefu kutokana na ukweli kwamba Gazeti hilo
mrengo wake unafahamika kuwa ni wa ukosoaji.
Akizungumzia dhana ya
uhuru wa habari, Dkt. Abbasi amesema kuwa ipo haja ya wadau wa habari kufahamu
dhana halisi ya uhuru wa habari badala ya kuendelea kufanya makosa ya tafsiri isiyo
sahihi jambo ambalo linapotosha dhana nzima ya uhuru wa habari.
Dkt. Abbasi amesema
kuwa Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 1966 wa Haki za Kiraia na Kisiasa, ibara ya
19 inaeleza haki za kupata habari ambayo inaenda sambamba na ukomo wa kutoa
taarifa kwa maslahi ya nchi.
Aidha Dkt. Abbasi
ametoa rai kwa wadau wa habari nchini kuisoma sheria ya huduma za habari ya
mwaka 2016 iliyoanza kutumika rasmi badala ya kuyaachia makundi ya wanaharakati
wapotoshe uhalisia wake.
Akizungumzia utekelezaji
wa Sheria hiyo, Dkt. Abbasi amesema kuwa sheria imekwishaanza kutekelezwa
katika hatua kadha ambapo alizitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na
utoaji wa Vitambulisho vya Waandishi wa Habarr.
Alisema kuwa utoaji wa
Vitambulisho hivyo umelenga kuwajengea uwezo wa kujiendeleza waandishi wa
habari katika kipindi cha mpito cha miaka mitano ili kufikia vigezo stahiki vya
taaluma.
Tanzania imeingia
katika Historia baada ya kutunga Sheria na 12 ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016
ambayo imefuta Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 ambayo imepitwa na wakati
kutokana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na utamaduni.
No comments:
Post a Comment