WAKATI nyota kutoka nchini Ivory
Coast Ibrahima Fofana, akianza majaribio leo, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki
na Kati, Azam FC imempokea straika mwingine raia wa Niger, Mossi Moussa Issa.
Issa ametua nchini usiku wa kuamkia
leo na ataanza rasmi majaribio kesho Jumamosi akiungana na Fofana, ambao wote
wanawania nafasi ya kusajiliwa na mabingwa hao kwa ajili ya msimu ujao.
Straika huyo ametokea timu ya Sahel
Sporting ya Niger, alikofunga mabao manne ndani ya mechi nane alizocheza pia
amewahi kucheza kwa mabingwa wa Morocco FUS Rabat mwaka 2013 na AS Douanes
(Niger).
Akizungumza mara baada ya kufika
makao makuu ya Azam Complex, Chamazi na Ofisa Mtendaji Mkuu Saad Kawemba, Issa
alisema amefarijika sana kupata nafasi ya kuja Azam FC kuonyesha kipaji huku
akidai kuwa amejipanga kupambana ili kusajiliwa na timu hiyo.
“Nimejiandaa vizuri na nipo asilimia
100 kupambana kupata nafasi hiyo ya kusajiliwa,” alisema kwa ufupi Issa.
Zeben anena
Naye Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben
Hernandez, alisema kuwa anatarajia kumwangalia mchezaji huyo kwenye mazoezi ya
kesho Jumamosi baada ya leo kuanza kumtazama Fofana.
“Leo nimeanza kumwangalia mchezaji
aliyefika juzi (Fofana), kesho nitamwona pia mchezaji mwingine (Issa),
nitawaangalia kwa kipindi kifupi kilichobakia na hapo ndipo nitakuja na maamuzi
ya mwisho,” alisema.
Katika hatua nyingine kocha huyo wa
zamani wa Santa Ursula ya Hispania, alisema kuwa mara baada ya mchezo wa
kirafiki dhidi ya Ashanti United Jumapili ijayo, anatarajia kutoa hatima ya
makipa wawili Mghana Daniel Yeboah na Mhispania Juan Jesus Gonzalez waliokuwa
kwenye majaribio ya kujiunga na Azam FC wakiwania nafasi moja ya usajili wa
golikipa.
Mechi mbili za kirafiki
Akizungumzia mechi za kirafiki
itakazocheza Azam FC, Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema kuwa timu
hiyo itaanza kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki keshokutwa Jumapili saa 3
asubuhi dhidi ya Ashanti United kabla ya kuvaana na timu ya Halmashauri ya
Kinondoni (KMC) Jumatano Ijayo.
No comments:
Post a Comment