Friday, 30 March 2018

MGODI ULIOUA WACHINA MKOANI GEITA WAFUNGWA



Mgodi  wa dhahabu katika Kijiji cha Nyamtondo wilayani na mkoani Geita umefungwa baada ya raia wawili wa China kufariki ndani ya shimo lenye urefu wa zaidi ya mita 100 kwa kulipukiwa na baruti wakati wakivunja miamba.
Wachina hao, imeelezwa, walikuwa wakivunja miamba ya dhahabu katika mgodi huo bila ya kuwa na vyeti vya kulipiua baruti.

Mgodi huo unamilikiwa kwa ubia baina ya Mayala Ngweso na kampuni ya Kichina ya Taichangain Tanzania Group.Akitoa tamko la kufunga mgodi jana, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Geita, Alli Maganga alisema hatuahiyo inalenga kupisha uchunguzi wa kina.

Pia, alisema Maganga, hatua hiyo itashinikiza mgodi huo kutekeleza masharti na maelekezo uliopewa na serikali ili kuhakikisha sheria na kanuni za madini zinazingatiwa na kufuatwa.

Maganga alisema raia wawili wa China waliotambuliwa kwa majina ya Li Shaobin (44) na Qian Zhaorang (49)waliojitambulisha kuwa mafundi michundo walifariki dunia baada ya kujeruhiwa vibaya na baruti ndani ya shimo katika mgodi huo wakilipua miamba ya dhahabu.

Alisema uchunguzi wa awali ulibaini marehemu hao hawakuwa na vyeti vinavyowaruhusu kulipua baruti, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria ya nchi.

Idara ya Madini ilifahamu kuwapo kwa tukio hilo baada ya uongozi wa mgodi kutoa taarifa ya ajali hiyo kwa mamlaka husika, alisema Maganga, Maganga alisema Sheria ya Baruti nchini inazuia mtu yeyote kulipua baruti bila ya kuwa na kibali.

Awali, akithibitisha kutokea kwa vifo hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lotson alisema chanzo cha ajali ni uzembe na kutahadharisha wamiliki wa migodi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na tahadhari ili kupeukana na jali zisizo za lazima.

Oktoba 10, mwaka jana mchimbaji mmoja alifariki dunia na mwingine kunusurika baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika mgodi wa dhahabu usio rasmi wa Bingwa, katika kijiji cha Rwamgasa wilaya na mkoa wa Geita usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Lodson, alimtaja aliyefariki kuwa ni Fikiri Paulo (27), mkazi wa kijiji cha Mlanda wilayani Chato ambaye mwili wake ulitolewa shimoni akiwa ameshaaga dunia.


Mwili huo ulitolewa shimoni na wachimbaji wadogo, kwa mujibu wa mkurugenzi wa mgodi wa Bingwa, Hussein Nyanzala.
Nyazala alisema walikesha wakiendesha zoezi la kuufukua mwili wa marehemu kuanzia saa 5:00 usiku ajali ilipotokea hadi saa moja asubuhi.

Kamanda Mponjoli alimtaja manusura wa ajali hiyo kuwa ni Musa Evarist (19), mkazi wa kijiji cha Mpomvu.Alisema Evarist aliokolewa muda mfupi baada ya kufukiwa na kifusi wakati wakichimba mwamba.

Chanzo cha ajali hiyo kilidaiwa kuwa ni kukatika kwa gema la udogo wa mwamba wa mawe katika shimo walimokuwa wakichimba vijana hao, Baada ya gema kukatika, imeelezwa, kifusi kilifukia wachimbaji hao.

No comments:

Post a Comment